HabariLifestyleNews

Siku ya Kimataifa ya Vijana; Vijana Washinikiza Viongozi Kuwapa Nafasi za Kuongoza Kuliimarisha Taifa Kimaendeleo

Na huku Ulimwengu ukiadhimisha siku ya Kimataifa ya Vijana (IYD2024), Kenya imejiunga na mataifa mengine kuadhimisha siku hii huku wito ukitolewa kwa viongozi kuwaimarisha vijana kimaendeleo.

Maadhimisho haya yanajiri chini ya miezi miwili tangu kuzuka kwa wimbi la maandamano ya kuipinga serikali dhidi ya uongozi mbaya.

Maandamano hayo yaliyoongozwa na vijana wa kizazi cha Z maarufu Gen Z kote nchini, yalishinkiza mageuzi na uongozi bora sawia na kutaka kusikilizwa kwa vijana.

Peter Karisa mmoja wa viongozi wa vijana eneobunge la Magarini kaunti ya Kilifi anasema kuwa vijana hawajatambulika vilivyo katika masuala ya ajira, akisema kuwa hatua hiyo imepelekea wengi wao kujihusisha na vitendo viovu ikiwemo utumizi wa mihadarati na hata kutumiwa vibaya.

Vijana hawajatambulika vilivyo hasa masuala ya ajira, wengi wako mitaani wanajihusisha mambo maovu, dawa za kulevya kwa sababu kukosa ajira. Mara nyingi wanasiasa wanawatumia vijana vibaya wakati wa kampeini na kuzua vurugu halafu wanawaacha.” Alisema

Karisa alikariri kuwa Imefika wakati vijana nao wamepewe fursa ya uongozi katika nyanja na idara mbali serikalini ili kuonyesha ujuzi na tajriba waliyo nayo.

“Si lazima uongozi kupitia kupigiwa kura debeni, lakini uongozi uko sekta tofauto tofauti na hali nyingi kama ni kusimamia mahali au miradi fulani acha vijana wapewe nafasi kushikilia sekta hizo na waonyeshe kweli wako na uwezo.” Alisema.

Huku hayo yakijiri, Mbunge wa Matuga Kassim Sawa Tandaza aliwahimiza vijana kujiunga na vyuo vya kiufundi katika eneo hilo kusomea taaluma mbalimbali na kupata ujuzi wa kujiajiri.

Nawataka vijana wasidharau wajitokeze kwenye hizi taasisi za kiufundi, TVETs wasomee kozi hizi kuanzia artisan wapate certificate na kisha watapanda wawe na ujuzi wa kujitegemea na kujipatia ajira.” Alisema.

MJOMBA RASHID