HabariNews

COTU Yamtahadharisha Waziri mpya wa Fedha Dhidi ya Masharti tata ya IMF

Chama cha kutetea maslahi ya Wafanyakazi nchini, COTU kimemwonya Waziri mpya wa Fedha John Mbadi kuhusu kuchukua tahadhari katika kutekeleza mapendekezo ya kiuchumi ya Shirika la Kimataifa la Fedha, IMF.

Katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari, Katibu Mkuu wa COTU Francis Atwoli ameeleza wasiwasi wake kuhusu athari mbaya zinazoweza kutokea za kufuatiliza masharti makali ya IMF katika uchumi wa Kenya, haswa kwa maisha ya raia na wafanyikazi.

Atwoli ametaja matukio ya awali ambayo yalionyesha athari mbaya zilizojitokeza kwa kufuatilia kikamilifu ushauri wa IMF bila ya uhakiki, akimsihi Waziri Mbadi kufuatilia mapendekezo ya IMF kwa umakini na ufahamu wa kina wa athari zake kwa wananchi wa kawaida.

Chama hicho cha wafanyakazi kimepigia mfano enzi za hatamu ya uongozi wa rais wa 3 hayati Mwai Kibaki, jinsi alivyoweka usawa katika kufuatilia mapendekezo na masharti ya IMF huku ikiyaweka maslahi ya Wakenya kama kipaombele kikuu.

COTU sasa ikionya kuwa sera hizo za masharti magumu ya Shirika hilo la fedha duniani zinaweza kupelekea machafuko na maandamano kote nchini na hata kuzidishia matatizo ya kifedha na kiuchumi kwa raia kutaabika zaidi kimaisha.

Kulingana na COTU, utekelezaji wa asilimia 100 wa marekebisho ya kiuchumi na kifedha pasi kuzingatia muktadha na mahitaji ya ndani ya nchi, kunaweza kusababisha kushindwa, huku ikitaja kuwa masharti ya IMF mara nyingi huhusisha mikakati ambayo huwalemea wananchi kupitia ongezeko la ushuru na hatua za kubana matumizi.

Kauli yake Atwoli inajiri kufuatia mkutano wa leo kati ya waziri wa Fedha John Mbadi na Mwakilishi wa IMF nchini Kenya, Selim Cakir.

Mkutano uliothibitishwa na Wizara ya fedha kwenye mtandao wake wa X umefanyika kabla ya IMF kutoa mkopo zaidi ya bilioni 181.

By Mjomba Rashid