HabariNews

Mabingwa wa Olimpiki Wapongezwa; Rais Akisisitiza Matumizi Mwafaka ya Fedha za Michezo

Rais William Ruto amemwagiza Waziri wa Michezo Kipchumba Murkomen kuhakikisha kuwa Hazina ya fedha za michezo inatumiwa vilivyo katika sekta hiyo.

Akizungumza katika Dhifa ya asubuhi iliyoandaliwa katika Ikulu ya Eldoret, kuwakaribisha wanariadha walioshiriki michezo ya Olimpiki nchini Paris, mnamo siku ya Alhamisi Rais Ruto amesema kubuniwa kwa hazina hiyo ilikuwa kwa malengo ya kuwasaidia wanamichezo wote nchini ili kuimarisha miundomsingi ya michezo sawia na kuwapa motisha wanamichezo wote.

Nimetoa maagizo mwafaka na ya kueleweka kwa bwana Waziri katika ofisi yako, hazina hii ya fedha za michezo ni ya wanamichezo wote. Kuimarisha moundomsingi ya michezo, kuwaimarisha wanamichezo, kuwatambua a kuwaweka hali salama, fedha hizi ziwape motisha kuhakikisha wanafanikiwa.”

Rais amesema kulikuwa na jaribio la kutumia fedha za hazina hiyo kwa masuala mengine hivyo basi kuwepo haja kwa Waziri husika kuhakikisha fedha hizo zinafaidi sekta ya michezo vilivyo.

Ndio sababu kwa nini tuliunda hazina ya fedha za michezo mwaka 2022, fedha zisitumike kwa mambo mengine kando na michezo, kulikuwa na jaribio la kutumia na kusambaza fedha hizi kwa mambo mengine kando na michezo. Fedha hizi ni za wanamichezo wetu ziwasaidie.” Alisema.

Na licha ya baadhi ya wanariadha kushindwa kufanya vyema kinyume cha matarajio ya Wakenya hasa akiwemo Eliud Kipchoge ambaye hakumaliza mbio za marathoni, Rais amewasifia wanariadha hao kwa ushindani wao waliouonesha akiwataka wakenya wawape moyo kwa hatua walizopiga.

Eliud ni gwiji mkubwa sana na najua wengi walivunjika moyo wakijiuliza maswali kwa nini Eliud alishindwa kumaliza mbio. Lakini tunakutambua na tunakusherehekea wewe na wanariadha wetu wengine.

Tafadhali Wakenya tuwaadhimishe na kuwasherehekea wanariadha wetu, tusiwakashifu sana, wanafanya mengi sana na kujitolea kufanya bendera yetu ipepee katika Miji mikubwa ote Ulimwenguni.” Alisema.

Rais aidha amesema wanariadha hao wameiletea nchi heshima na ushindi ikilinganishwa na mataifa mengine barani Afrika ambayo hayakufanya vyema.

Wameleta ushindi kwa nchi yetu na tunasherehekea hapa. Si mliona jinsi sherehe walivyofanya kule Botswana na wana medali moja tu ya dhahabu, moja tu! Na sisi hapa tuna nne, na unaona wengine wameandika huko wanakashifu ooh timu yetu haikufanya vyema. Kati ya medali 8 za dhahabu zilizokuja Afrika sisi tuna nne, hili si la kudharauliwa kabisa. Alisema Rais

Wanariadha waliowakilisha Kenya katika Makala ya 33 ya michezo ya Olimpiki huko Paris Nchini Ufaransa wameandaliwa dhifa ya asubuhi na mapokezi rasmi karika Ikulu ya Eldoret.

Kenya ilizoa medali 11, zikiwemo 4 za dhahabu, 2 za fedha na 5 za shabahuku wote waliopata medali wakitarajiwa kukabidhiwa na serikali shilingi milioni 5.

By Mjomba Rashid