Jamaa mmoja wa umri wa miaka 24 ameuawa na umati wenye ghadhabu huko Magarini kaunti ya Kilifi baada ya kumwua baba yake.
Ismail Karisa Mwaiha amepokea kichapo kutoka kwa umati huo hadi kufa baada ya kumtendea unyama huo baba yake mzazi Karisa Mwaiha.
Inadaiwa Ismail alitaka kutunda ndimu shambani kabla babaye kumkataza, hatua iliyompelekea kumvamia babake na kumwua kwa kumkatakata kwa panga.
Hata hivyo Umma uliojawa na ghadhabu ulimvamia Ismail na kumpiga hadi kumuuwa wakimtaja kuwa mtu asiyekuwa na maadili.
Umati huo umedai kuwa kwa muda mrefu kijana huyo amekuwa akimdhalilisha mzazi wake huku Kwa mara mbili akishtakiwa na kutumikia kifungo gerezani.
Akithibitisha kisa hicho kamanda wa polisi Kaunti ya Kilifi Fatma Hadi amelaani vikali kitendo hicho akiwataka wakaazi kutafuta njia mbadala kusuluhisha mizozo yao badala ya kuchukua hatua mikononi mwao.
Hadi amesema tayari maafisa wake wameanzisha uchunguzi mkali kuhusu kisa hicho akionya yeyote atakayepatikana kuwa atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Miili ya wawili hao imepelekwa katika hifadhi ya maiti ya hospitali ya Malindi ikisubiri kufanyiwa upasuaji kwa ajili ya uchunguzi.
By Joseph Yeri