Mahakama ya Leba imeagiza kusitishwa kwa muda mgomo wa walimu wanachama wa KUPPET ulioanza siku ya Jumatatu.
Hii ni baada ya kesi kuwasilishwa mahakamani na Tume ya Walimu TSC.
Jaji James Rika wa mahakama hiyo amesema masuala yaliyowasilishwa mbele yake na TSC ni ya muhimu na yana uzito hivyo kwataka walimu hao kusitisha mgomo wao kwa sasa hadi kesi hiyo itakapoamulwa.
Jaji Rika aidha ameiagiza KUPPET na Wizara ya Leba kuwasilisha majibu yao katika kesi hiyo ndani ya siku 7.
Kesi hii itatajwa tarehe tano mwezi Septemba mwaka huu.
Itakumbukwa walimu wanachama wa KUPPET walianza rasmi mgomo wao wa kitaifa katika siku ya kwanza ya Muhula wa tatu baada ya Serikali kushindwa kuangazia lalama zao, huku walimu hao wakiapa kutorejea shuleni hadi pale matakwa yao yatakapotekelezwa.
BY MJOMBA RASHID