Ukosefu wa ajira umetajwa kuchangia kwa kiwango kikubwa visa vya watu kujitoa uhai kaunti ya Kilifi, kutokana na wengi kushindwa kukidhi mahitaji yao muhimu na yale ya familia zao. Hali inayoelezwa kupelekea wakazi kupatwa na matatizo ya afya ya akili na hatimaye kujitoa uhai.
Visa vya watu kujitoa uhai vikiendelea kushuhudiwa kaunti ya Kilifi hamasa inazidi kutolewa kwa jamii kushirikiana na kusaidiana kimawazo pamoja na kupeana ushauri nasaha ili kukabiliana na visa hivyo na kuepusha vifo zaidi.
Chea Kingi msimamizi wa afya ya akili eneo bunge la Kilifi kaskazini, anasema takwimu kutoka kwa kamishna wa kaunti ya Kilifi kuanzia mwezi Machi mwaka 2023 hadi Agosti mwaka 2024 jumla ya visa 59 vya watu kujitoa uhai viliripotiwa huku eneo bunge la Malindi likiongoza kwa visa vingi zaidi vya watu kujitoa kwa kuripoti visa 15, Kilifi kusini visa 14 huku Kilifi kaskazini ikiripoti visa 10.
“Gatuzi dogo la Malindi linaongoza kwa visa hivi vya watu kujitoa uhai ikiripoti visa 15, ikifuatiwa na Kilifi kusini kwa visa 14 na Kilifi kaskazini ikiripoti visa 10 vya watu kujitoa uhai.Hii ni ile takwimu ya visa vilivyoripotiwa na kuna vile visa ambavyo viko huko mashinani na havikuripotiwa ambavyo ndio vingi mno kwa hivyo hili tatizo ni kubwa mno kwetu nan i vyema tuje pamoja tulizungumzie” alisema Kingi
Kingi, ameeleza kuwa chanzo kikuu cha ongezeko la visa hivyo siku za hivi karibuni ni ukosefu wa ajira kwa wakazi hali inayowapelekea wengi kukumbwa na matatizo ya afya ya akili yanayowasukuma kujitoa uhai.
“Vitu ambavyo huwa vinachangia sana katika hali hizi za mtu mpaka aweze kujitoa uhai, ile kubwa zaidi ambalo tumeliona hivi karibuni ni ukosefu wa ajira. Ukosefu wa ajira umechangia pakubwa kwa msukumo wa watu kujitoa uhai.” alisema Kingi.
Job Monyoncho ofisa wa shirika la Basic Needs Basic Rights Kenya, anasema hamasa inayotolewa inaendelea kuzaa matunda kufuatia wakazi kutafuta usaidizi hospitalini wanapokumbwa na changamoto ya msongo wa mawazo na kiwewe.
Hata hivyo ameongeza kuwa kupitia wafadhili mbali mbali shirika hilo linapanga mikakati ya kuhakikisha kuwa dawa za kutibu matatizo ya afya ya akili zinapatikana hospitalini kwa bei nafuu.
“Tangu tulipoanza mpaka sasa hivi, tunakuta ni watu wengi ambao wanakwenda kutafuta huduma hizi au usaidizi hospitali, na hilo tunasema ni ushindi kwetu. Na sisi hata kuendelea kwa usaidizi wetu kwa jamii tumeongea na wafadhili wetu nao wametusaidia kutafuta dawa za matatizo ya afya ya akili kwasababu dawa hizi ziko ghali na pia hazipatikani kwa urahisi kwa yule mkaazi wa chini.
“Wakati mwengine pia tunasambazia dawa baadhi ya hospitali zetu ili wakazi wetu wakifika hospitali wakiandikiwa dawa waweze kuipata kwa bei nafuu ikilinganishwa na maduka ya kuuza dawa.” alisema Monyoncho.
Erickson Kadzeha