HabariNews

Serikali yatakiwa kuwaachilia huru walioshtakiwa na kufungwa gerezani kwa kosa la kukamatwa na bangi.

Serikali imetakiwa kuwaachilia huru wafungwa walioshtakiwa na kesi za kukamatwa na bangi ama kuwabadilishia adhabu ili kuwawezesha wafungwa hao kuwa karibu na familia zao.

Kwa mujibu wa profesa George Wajackoyah kinara wa chama cha siasa cha Roots, kuna wafungwa zaidi ya elfu 70 humu nchini walioshtakiwa na makosa ya kukutwa na bangi, akieleza kuwa tayari amemuandikia barua waziri wa usalama profesa Kithure Kindiki kumsihi kuwaachilia huru wafungwa hao.

Akizungumza mjini Kilifi amesema serikali inafaa kutumia hela za kuwazuilia wahalifu kufanyia miradi ya maendeleo huku wahalifu hao wakipewa adhabu nyingine ambazo zitaweza kuwaweka karibu na familia zao.

“Hapa Kenya tuko na kesi zaidi ya elfu zinazohusu wahalifu wa bangi na nimemuandikia barua waziri wa usalama profesa Kindiki lakini bado hajanijibu. Mtu anashikwa na msokoto mdogo wa bangi na anafungwa gerezani na zile pesa zinazotumika kukuhudumia wewe kule gerezani ni ushuru wa Wakenya kosa ambalo linafaa kuwa dogo tu lakini unafungwa gerezani ni kama mtu aliyetenda kosa la uhaini.

“Ningependa serikali iwawachilie hawa na ikiwa inaona hiyo adhabu haitoshi basi wawape hata adhabu ya kufanya kazi mitaani ili waweze kuwa karibu na familia zao.” alisema Wajackoyah.

Hata hivyo profesa Wajackoyah ameipendekezea serikali kutafakari upya wito wake wa kuruhusu upanzi wa mmea wa bangi kwa ajili ya kusafirisha nje ya nchi ili kuikwamua nchi kutokana na malimbikizi ya madeni kutoka kwa mataifa mengine.

Pia amesistiza kuwa hamasa ya kutosha inafaa kutolewa kwa wananchi ili kuondoa tashwishwi inayohusishwa na mmea huo na kuangazia manufaa yanayotokana na mmea huo huku akieleza kuwa mataifa mengi sasa hivi yamekuwa yanatumia fibre zinazotokana na mmea wa bangi katika kutengeneza bidhaa zao.

“Unajua watu wengi hawaelewi. Watu wakiskia bangi wanafikiria ni ile ya kuvuta. Kuna ule mmea ambao unaitwa hermp ambao unamatumizi aina tatu tofauti. Kuna matumizi ya nyumbani ambapo inatengenezwa bidhaa kama vile mafuta ya nywele za wanawake, mafuta ya kutengeneza dawa za kutibu saratani, pia inatumiwa kutengeneza fibre.

“Taifa la Rwanda juma lijalo litafungua kiwanda cha kutengeneza hermp kwa bidhaa mbali mbali na utaona uchumi wao unaweza kuimarika mara 12 zaidi ya Kenya. Mataifa mengi sasa yameanza kususia utenengezaji wa bidhaa zao kutumia fibre ya pamba na kukumbatia fibre ya hermp ambayo ni bora zaidi ya ile ya pamba.” alisema Wajackoyah.

Caleb Otieno kiongozi wa vijana mjini Kilifi ametoa wito kwa serikali kuelekeza katika miradi mingine pesa zinazotumiwa kupambana na utumizi wa bangi nchini iwapo serikali haijaandikisha mafanikio makubwa dhidi ya utumizi wa bidhaa hiyo huku akilitaka shirika la afya duniani WHO pamoja na serikali ya taifa hili kutoa taakwimu za watu walioathirika kwa utumizi wa bangi pamoja na uvutaji wa sigara.

“Ndio maana tunataka kuwauliza shirika la afya duniani watueleze ni watu wangapi wameathirika na utumizi wa bangi ikilinganishwa na uvutaji sigara? Na kwa serikali ya taifa letu tunataka kujua tangu mwaka 1964 ni pesa ngapi zimetumika kuendeleza vita dhidi ya utumizi wa bangi na je, kuna taarifa zozote za mafanikio ya kumaliza utumizi wa bangi? Basi ikiwa hakuna itakuwa ni muda mwafaka wa serikali kurudi tena kwenye kuweka mikakati mipya.” alisema Otieno.

By Erickson Kadzeha