HabariNews

Walinzi wa Jaji aliyemhukumu jela Kaimu Inspekta Jenerali wa Polisi Waondolewa

Walinzi wa Jaji wa Mahakama Kuu Lawrence Mugambi wameondolewa.

Uamuzi huu unajiri siku mbili tu baada ya jaji huyo kumhukumu Kaimu Inspekta Jenerali wa Polisi Gilbert Masengeli kifungo cha miezi 6 gerezani.

Masengeli alikaidi maagizo ya mahakama na kukosa kufika mahakamani mara saba alipohitajika Kwenda kueleza waliko wanaume watatu waliotekwa nyara huko Kitengela.

Katika ripoti yake Jaji Mkuu nchini Martha Koome amethibitisha hilo akisema walinzi wa jaji huyo walinyang’anywa silaha zao na kisha kuondolewa wikendi iliyopita.

Hatua ya kuvunja moyo ilitekelezwa na Idara ya Polisi kufuatia kuhukumiwa jela kwa kaimu Inspekta Jenerali. Maafisa wa polisi wanaomlinda Jaji Mugambo walipokonywa silaha na kisha kuondolewa wikendi,” alisema Koome.

Akikashifu kitendo hicho Koome amesema hatua hiyo ya Huduma ya Polisi ni kinyume cha katiba kwa mujibu wa kipengee 160 kinachohimiza uhuru wa idara ya Mahakama.

Ameitaka Idara ya Polisi iwarejeshe walinzi wa jaji huyo mara moja huku akiwahikikishia wakenya kuwa Idara ya mahakama itasimama imara kulinda sheria na kwamba hatatishiwa na idara ya polisi hata kidogo.

Kitendo cha Idara ya Polisi ni cha hujuma na kutaka kututishia, na hatutakubali. Tutasimama imara kulinda haki na sheria,” alisema.

By Mjomba Rashid