HabariLifestyleNews

IPOA Kuchunguza Kitendo cha Kuondolewa kwa Walinzi wa Jaji wa Mahakama Kuu

Mamlaka Huru ya Kutathmini Utendakazi wa Polisi nchini (IPOA) imeanzisha uchunguzi wa madai ya kuondolewa kwa walinzi wa Jaji wa Mahakama Kuu Lawrence Mugambi na pia visa vya baadhi ya viongozi kutoka idara hiyo ya polisi kupuuza amri zinazotolewa na mahakama.

Katika taarifa yake IPOA imesema imechukua hatua hiyo ili kuhakiksha kuwa sheria zinafuatwa na maafisa wa idara ya polisi wakiwemo viongozi wa ngazi ya juu wa idara hiyo Kulingana na IPOA uchunguzi huo utafanyika kwa mujibu wa kipengee cha 6 cha sheria 86 za mamlaka hiyo ambacho kinatoa kibali cha kufunguliwa mashtaka afisa yeyote anayekiuka sheria za nchi, sasa mamlaka hiyo ikisema hakuna atakayesazwa kwenye uchunguzi huo.

Kauli ya IPOA inajiri siku moja tu baada ya Tume ya Huduma za mahakama (JSC) kutoa taarifa ikalalamikia tukio la jaji Mugambi kunyang’anywa walinzi wake na pia amri za mahakama kupuuzwa na viongozi wa ngazi ya juu serikalini haswa waliopo katika idara ya polisi.

Itakumbukwa kuwa Hakimu Lawrence Mugambi alinyanganywa walinzi wake siku tatu tu baada ya kumuhukumu kaimu inspekta mkuu wa polisi Gilbert Masengeli kifungo cha miezi sita baada ya kupatikana na hatia ya kudharau mahakama kwa kukaidi maagizo yake.

Hata hivyo saa kadhaa baada ya IPOA kutangaza kuanza uchunguzi wa hatua ya kuondolewa walinzi kwa jaji huyo, Kaimu Inspekta Jenerali wa Polisi Gilbert Masengeli amejitokeza na kukana madai hayo kama ilivyotangazwa na Tume ya Huduma za Mahakama, JSC.

Masengeli hata hivyo katika kile kinachoonekana ukaidi amesisitiza kuwa hatashurutishwa na yeyote kutekeleza majukumu yake ambayo ni pamoja na kuwaajiri, kuwatuma na kuwaondoa maafisa wa polisi. Amesema kuwa idara ya polisi NPS, ni idara huru na ina majukumu ya kuhakikisha kuwa kila mkenya anapata ulinzi.

BY NEWS DESK