HabariNewsSiasa

Seneta wa Tana River Awasilisha Mswada Bungeni Kujadili Hoja ya Kutokuwa na Imani na Naibu Rais

Seneta wa Tana River Danson Buya Mungatana amewasilisha mswada katika bunge la Seneti kujadili hoja ya kutokuwa na imani na Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Akiongea na wanahabari Mungatana amesema Gachagua ameonesha mienenendo potovu na amekiuka vipengee vya sheria kuhusu jinsi anavyofaa kutekeleza majukumu yake, huku akimshtumu kwa kupuuza kiapo chake cha afisi.

Mungatana amesema naibu huyo wa rais amekuwa akipotoka kimaadili tangu kuchukua wadhfa huo kwa kuendelea kutoa semi ambazo zimeleta migogoro na migawanyiko miongoni mwa Wakenya.

Seneta huyo amesema Gachagua amekuwa kiongozi wa kikabila na kimaeneo kinyume cha katiba inavyomtaka kuwa, akimtaja kujihusisha na siasa za Mlima Kenya na kuwatenga Wakenya wa maeneo mengine tofauti na kipengee cha 75 cha katiba kinachoainisha jinsi kiongozi wa kitaifa anavyostahiki kuwa.

Kulingana naye Bunge la Seneti halijafurahishwa kamwe na mienendo yake ikizingatiwa wadhfa anaoshikilia serikalini.

By Mjomba Rashid