Ukosefu wa kupata ushauri nasaha,jamii kutojadili mwafaka na kutowekwa karibu na familia ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazotajwa kuwakumba waathiriwa wa visa vya dhulma za unyanyasaji wa kingono zinazowapelekea waathiriwa hao kuchukua muda mrefu kupona na kuendelea na maisha yao kawaida.
Ukosefu huo wa msaada hitajika kama vile ushauri nasaha kwa waathiriwa wa dhulma za kingono umechangia kushuhudiwa kwa visa vya watu kujitoa uhai.
Kwa mujibu wa Esther Njuguna, mkurugenzi mkuu wa huduma kwa manusura wa shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la IJM ambaye pia ni mtaalamu wa akili, jamii imekuwa ikifumbia macho vitendo hivi na kupuuzilia mbali kujadili jinsi ya kupata mwafaka wa kuwasaidia waathiriwa kurudi katika hali zao za kawaida baada ya kupitia uovu huo hali inayowafanya waathiriwa kuhisi kutotambuliwa na kukosa utetezi.
“Mara nyingi huanza na jamii vile tunavyoangalia maswala ya ushauri, vile tunavyoangalia maswala ya kuwasaidia waathiriwa. Tunakosa kupeana mazingira mazuri ya mwathiriwa kupona badala yake tunalazimisha kuyasahau madhila waliyopitia hususan visa vya unyanyasaji wa kingono hatutaki kabisa kuyaongelea. Hali hii inafanya mwathiriwa kutojihisi sawa kuzungumza aliyopitia ili aweze kupona.” alisema Bi.Njuguna.
Aidha ametoa wito kwa washauri nasaha kutoa hamasa zaidi kwa jamii ili wafahamu umuhimu wa kutafuta huduma za ushauri pia kuitumia kama mbinu ya kuonesha mshikamano kwa waathiriwa wa visa hivyo jambo analodai kuwa litasaidia kupungua kwa visa vya watu kujitoa uhai.
“Kwa hivyo sisi wataalamu tuendelee kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa ushauri nasaha na ule msaada ambao ni wapewe waathiriwa kutoka kwetu sisi waatalamu ili wasaidike.” alisema Bi. Njuguna.
Simon Kazungu ofisa wa shirika la Kilifi Social Justice Centre ameeleza kuwa visa vingi vya unyanyasaji wa kingono ambavyo waathiriwa wamepitia vimemefanywa na wanafamilia huku akiongeza kuwa kukosekana kwa ushirikiano kutoka kwa familia kumezidisha changamoto ya kupatikana haki kwa waathiriwa.
Ameongeza kuwa waathiriwa wengi wa visa vya unyanyasaji wa kingono ni watoto wa shule jambo linalo aminika kuathiri sekta hiyo ya elimu.
“Sekta ambayo imeathirika zaidi ni ya elimu kwasababu waathiriwa wengi ni watoto wa shule na utakuta kwamba wamefanyiwa visa hivi na watu wa familia ama walimu.” alisema Kazungu.
Erickson Kadzeha