Waziri wa masuala ya kitaifa na usalama wa Ndani Kithure Kindiki amejitenga na mjadala unaotokota wa kutaka kumbandua Naibu Rais Rigathi Gachagua na badala yake amehimiza umoja.
Akizungumza huko Kaunti ya Nyandarua wakati wa uzinduzi wa mradi wa barabara, Kindiki amesisitiza kujitolea kwa serikali katika kuendeleza umoja wa kitaifa na kukamilisha miradi ya maendeleo iliyokwama nchini.
Na huku akionekana kukwepa vuta nikuvute ya kisiasa iliyogubika uwezekano wa kubanduliwa kwa Naibu Rais, Waziri Kindiki amewasihi Wakenya kusalia na umoja pasi kujali tofauti za kikabila, kidini wala kijamii, na kujitolea kulitumikia taifa.
Waziri Kindiki aliyekuwa ameandamana na Waziri wa Uchukuzi na Barabara Davis Chirchir ameshikilia kuwa lengo la Serikali ni kuangazia ufanikishaji wa miradi ya kimaendeleo na kuimarisha miundomsingi.
Wakati uo huo Kindiki amewaagiza wanakandarasi wanaofanyia kazi miradi ya serikali kuwapa kipaombele wakazi wa maeneo husika walio na ujuzi ili kuhakikisha miradi inawafaidi wananchi mashinani.
By Mjomba Rashid