HabariLifestyleNews

Asilimia 30 ya wakazi kaunti ya Kilifi wapitia aina tofauti tofauti za ugomvi wa kijinsia

Serikali ya kitaifa na ile ya kaunti ya Kilifi kwa ushirikiano na ubalozi wa taifa la Denmark, imezindua rasmi kituo cha kwanza cha umma cha kuwanusuru waathiriwa wa visa vya ugomvi.

Kituo hicho kilichofunguliwa katika wadi ya Kibarani kaunti ya Kilifi, chini ya mpango wa kitaifa wa Accelerate, hii ikiwa miongoni mwa mikakati ya kukabiliana na visa hivyo.

Ufunguzi wa kituo hicho unatajwa kuwa mwanga wa matumaini kwa waathiriwa visa cya ugomvi hasa ikibainika kuwa asilimia 30 ya wakazi Kilifi hupitia aina tofauti tofauti vya ugomvi wa kijinsia.

Kilifi ikiorodheshwa miongoni mwa kaunti zilizo na visa vingi vya ugomvi wa kijinsia wito umetolewa kwa wakazi, mashirika ya kijamii na wadau mbali mbali kushirikiana katika kukabiliana na visa hivyo huku kaunti 13 zikijitokeza katika uzinduzi wa kituo cha kwanza cha umma cha kuwanusuru waathiriwa wa visa vya ugomvi wa kijinsia wadi ya Kibarani kaunti ya Kilifi.

Kwa mujibu wa naibu gavana wa Kilifi Florence Chibule Mbetsa, asilimia 30 ya wakazi kaunti ya Kilifi wamepitia aina tofauti tofauti za ugomvi wa kijinsia huku akitaja kuwa swala hilo limekuwa likikosa kuongelewa kwenye jamii.

Dkt. Margaret Njenga afisa mkuu mtendaji wa shirika la PS Kenya, ameeleza kuwa kupitia mpango wa Accelerate umeweza kutoa huduma kwa wanawake zaidi ya laki 7 kote nchini.

Ameongeza kuwa kupitia mpango huo wanawake wanapata hamasa ya jinsi ya kupanga uzazi katika vituo zaidi ya 400 ili kuwasaidia kuishi maisha bora.
Kiongozi wa ushirikiano katika maswala ya afya katika ubalozi wa taifa la Denmark humu nchini Henrick Larson amesema kukosekana kwa vituo vya kuwahifadhi waathiriwa wa visa hivi kumekuwa changamoto katika kutafuta kupona na kurudi katika maisha yao ya kawaida.
Mwenyekiti wa kituo cha Kimbilio Salome Karisa, anasema wasichana wengi wamekuwa wakidhulumiwa mitaani wakitafuta kujikimu kimaisha baada ya kufukuzwa nyumbani wanapopata ujauzito.
By Erickson Kadzeha.