Kesi imewasilishwa mahakamani kupinga uteuzi wa Inspekta Jenerali wa Polisi nchini Douglas Kanja.
Katika kesi hiyo iliyowasilishwa na Seneta wa Busia Okiya Omtatah pamoja na wakenya wawili Eliud Karanja na Magare Gikenyi wanahoji kuwa Kanja hakukabiliwa na mchakato shindani wa kuajiriwa na hivyo uteuzi wake unapaswa kutangazwa kuwa batili.
Omtatah amesema uteuzi huo wa Kanja uliotekelezwa na Rais Ruto ulikwenda kinyume na sheria na kwamba ulikuwa moja kwa moja badala ya kutoa fursa kwa wakenya kutuma ombi la kushikilia wadhfa huo.
Jaji Bahati Mwamuye amethibitisha suala la kesi hiyo kuwa la dharura na kuagiza waliotajwa katika kesi hiyo kukusanya na kuhifadhi taarifa zote na nyaraka ambazo wao na mashirikamengine ya umma wanashikilia kuhusiana na usahihi wa uteuzi wa Kanja, ukaguzi wake, kuidhinishwa na bunge hadi kuteuliwa rasmi.
Miongoni mwa waliotajwa katika kesi hiyo ni pamoja na Mwanasheria Mkuu Dorcas Odour, Bunge la Kitaifa, Seneti, Mamlaka Huru ya Kutathmini Utendakazi wa Polisi (IPOA), Idaraya ya Kitaifa Polisi (NPS), Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadam (KNCHR) na Douglas Kanja mwenyewe.
Itakumbukwa kuwa Kanja aliapishwa wiki jana kuhudumu kama Inspekta jenerali wa polisi baada ya bunge kumuidhinisha na kisha rais William Ruto kumteua rasmi. Kesi hiyo itasikilizwa Oktoba 15 mwaka huu.
By Mjomba Rashid