Kwa mara nyingine tena maafisa wa polisi wamelaumiwa kwa ukiukaji wa haki za kibinadamu kwa kupitia matumizi ya nguvu kupita kiasi.
Mashirika mbalimbali ya utetezi wa haki za kibinadam yakiongozwa na Amnesty International yamezidi kulimbikizia lawama maafisa wa idara ya polisi kutokana na hayo. Akihutubia wanahabari jijini Nairobi, wakati wa kutoa ripoti mpya ya maandamano ya kuingia Bunge mnamo Juni 25, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Amnesty International Hutton Irungu anasema hatua hiyo ya maafisa wa polisi ilipelekea vifo vya Wakenya 6 wengine zaidi ya 100 wakijeruhiwa walipohusika katika maandamano ya kuipinga serikali mwaka huu.
Ameeleza kuwa haikubaliki kamwe maafisa wa polisi kutumia nguvu kukabili waandamanaji wa amani badala ya kuwalinda huku akisisitiza kuwa haki ya kushiriki maandamano nchini imelindwa kikatiba. Ripoti hiyo mpya ya mashirika hayo inasema kutokana na maandamano hayo yaliyovurugwa na polisi kwa kutumia nguvu kuwatawanya, watu 72 hawajulikani waliko ikiwa ni kwa kupitia kutoweka kwa njia tatanishi au kwa kutekwa nyara.
Mashirika hayo yakiwemo lile la IMLU yalifanya uchunguzi kwa kuhoji walioshuhudia maandamano, sawia na kuchunguza kanda za video na picha zilizopigwa wakati huo na wataalam wao wa uchunguzi wakabaini kuwa polisi walizidiwa nguvu na waandamanaji na kuonekana kukosa mwongozo na mwelekeo
kwa kufyatua risasi kiholela.
Wameshtumu hatua hiyo walioitaja uzembe wa idara ya polisi nchini kwani walikuwa wamearifiwa siku kadhaa kuhusu kufanyika kwa maandamano hayo ya vijana wa Gen Z walioshinikiza mageuzi ya kiuchumi na kisiasa.
Kama sehemu ya juhudi zao za utetezi wa haki, Amnesty aidha imezindua mswada wa kutaka kubuniwa kwa Tume ya Mahakama ya Kuchunguza vifo, kupotea kwa watu na vitendo viovu vya maafisa wa polisi wakati wa maandamano. Mswada huo tayari upata saini 12,000 na utawasilishwa katika Bunge la Kitaifa katika siku zijazo.
By Mjomba Rashid