HabariNewsSiasa

Wabunge Walilia Usalama Kuimarishwa wakati wa kujadili hoja ya kumbandua Naibu Rais

Wabunge sasa wanataka kuhakikishiwa usalama wao wakati wa vikao vya kujadili hoja ya kumbandua uongozini Naibu wa Rais Rigathi Gachagua.

Mnamo Jumanne Oktoba 1, baada ya kuwasilishwa hoja hiyo, Kiongozi wa wachache bungeni Junet Mohammed alimtaka Spika Moses Wetangula kuwahakikishia usalama wabunge 291 waliotia saini hoja ya kubanduliwa uongozini Gachagua, akisema kuwa suala lililo mbele yao ni nyeti.

Junet alisema suala la kumbandua uongozini Gachagua ni mchakato utakaohitajia vikao kadhaa kabla ya hatima kuafikiwa, hivyo kuna haja wabunge kulindwa vilivyo hadi siku ya kupiga kura kwani kuna uwezekano wanaounga mkono hoja hiyo wakatishiwa maisha.

“Tunaomba bwana Spika uwahakikishie usalama wabunge wote 291 waliotia saini hoja hii, tunahitaji tuwaone wabunge wote wakati wa kupiga kura na kwa sababu ni mchakato bwana Spika sisi si wageni wa haya, ijulikane si chuki wala vita, tunafanya kazi yetu kisheria na kwa mujibu wa kaitba.”

Amemtaka Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja kuwajibikia usalama wa wabunge wote na kuwalinda dhidi ya vitisho na uwezekano wowote wa kuhujumiwa kutokana na msimamo waliochokua.

Tunataka Bw. Kanja tuliyeidhinisha hapa huko nyuma, atuhakikishie usalama suala hili ni zito na tusitishiwe tupewe ulinzi na usalama.” Alisema Junet.

Ni kauli iliyoungwa mkono na Kiongozi wa Wengi bungeni Kimani Ichung’wah aliyemtaka Spika Wetangula kumuagiza Inspekta Jenerali kuwalinda wabunge dhidi ya tishio la usalama wakati wa vikao vya kujadili hoja hiyo vitakapoanza rasmi hadi kukamilika.

Aidha katika kile kinachoonekana kuendeleza uhasama, Ichungw’ah ambaye amekuwa katika mgogoro na vita vya maneno kati yake na Gachagua ameitaja hoja hiyo kuwa nyeti na kuifananisha na vita vikali dhidi ya kiongozi mwenye roho katili.

Ichungwa akimwita Gachgaua kama mtu ‘asiye wa kawaida’ na mwenye ‘moyo mweusi.’

Kwa sababu Mhehsimiwa Spika nasema haya hasa baada ya taarifa na yalitokea Juni 25, na kama alivyosema Junet tunapambana na suala ambalo si la kawaida, hatushughulikii na mtu wa kawaida tunashughulika na mtu mweusi mwenye moyo mweusi,” alisema.

Haya yanajiri wakati Mbunge wa Mwingi Magharibi Mwengi Mutuse aliyewasilisha hoja hiyo ya kumbandua Gachagua yenye kurasa 100, akisoma majina ya wabunge waliotia saini hoja hiyo, na wabunge hao wanajumuisha wale wa mrengo wa upinzani wa Azimio la Umoja na wa mrengo tawala wa Kenya Kwanza.

Tayari Spika wa Moses Wetangua ameipokea hoja hiyo aliyoitaja kuwa imetimiza vigezo vyote hitajika vya kuwasilishwa na kujadiliwa.

By Mjomba Rashid