Washukiwa 26 wa uhalifu waliokuwa wamejihami kwa mapanga wanazuiliwa katika kituo cha polisi cha Diani kaunti ya Kwale, wakisubiri kufikishwa mahakamani.
Washukiwa hao wamekamatwa katika oparesheni ya pamoja ya asasi za usalama katika maeneo ya Kibundani, Kona ya Musa, Ibiza na Bongwe. Mwenyekiti wa kamati ya usalama ambaye pia ni naibu kamishna eneo la Msambweni Josphat Mutisya amesema kuwa washukiwa hao wenye umri wa kati ya miaka 14 hadi 21 walikwepa mkono wa sheria siku ya Jumapili kwa kuwakata kata mapanga
wenyeji baada ya kukamilika kwa mchuano wa kandanda katika uwanja wa Shamu.
“Sasa hawa 26 tumekamata tunawafikisha kortini kuwafungulia mashtaka, vijana wadogo sana hawa lakini sheria itafuata mkondo wake.”
Akiwahakikishia wakazi usalama imara, Afisa huyo amesema idara ya usalama haitaruhusu vijana wahuni kuendelea kuwahangaisha wananchi na kwamba wamezidisha doria na misako dhidi ya magenge ya vijana yanayotatiza usalama.
“Hawa vijana wanaoleta vurugu katika mji wetu hatutaruhusu, maafisa wote wako kila mahali kuhakikisha wanawafagia hawa vijana wote. Na tutaendelea na msako kuimarisha usalama.” Alisema.
Mutisya sasa ameitaka jamii kukomesha tabia za kuwatelekeza watoto wao na badala yake kuhakikisha wanapata haki msingi ya elimu kama njia moja wapo ya kutenga na tabia potofu.
By Bintikhamis Kadide