HabariLifestyleMombasaNews

Gavana Nassir Aitaka DCI kuharakisha Uchunguzi wa Kesi ya Ulawiti

‘Hakuna aliye juu ya sheria, kila mmoja anapaswa kufuata na kuzingatia sheria za nchi.’

Ni kauli yake Gavana wa Mombasa Abdulswamad Sharrif Nassir baada ya kujiwasilisha katika makao makuu ya Upelelezi ukanda wa Pwani, DCI Kuandikisha taarifa kuhusiana na kesi ya ulawiti wa mwanablogu mmoja.

Gavana Nassir ambaye amehusishwa na kesi hiyo anadaiwa kuwatuma vijana kumteka nyara na kumlawiti Bruce John Khajira, mwanablogu aliyemkashifu na hata kumtusi katika mtandao wa Tiktok.

Akizungumza na wanahabari baada ya kuandikisha taarifa kuhusiana na hayo, Nassir amesema amejiwasilisha mwenyewe kwa kuheshimu sheria na kwamba analaani masaibu yaliyomfika mwanablogu huyo.

Mimi mwenyewe kwa hiari yangu mwenyewe nimejileta, hakuna yoyote ambaye yuko juu ya sheria hiyo ielewe, nimejileta kama mfano hata mimi siko juu ya sheria. lazima haki iweze kupatikana kwa huyu kijana.” Akasema.

Gavana Nassir aidha ameitaka idara ya upepelezi DCI iharakishe kukamilisha uchunguzi ili mwathiriwa apate haki sawia na wahusika kukabiliwa kisheria.

Na vitendo kama hivi nimeomba DCI iweze kuharakisha wamalize hii ili kila kitu kiwe wazi na kijana aweze kupata haki yake.”

Mnamo siku ya Jumatatu Gavana huyo alivunja ukimya wake na kukanusha tuhuma za kuhusika katika hayo, akilaumu mahasimu wake wa kisiasa wanaoendeleza shutuma hizo kumharibia jina.

Itakumbukwa kuwa mwathiriwa Bruce John alidai kuwa mnamo Septemba 12 kundi la maafisa 20 wa kaunti walimteka nyumbani kwake Bamburi kwa kuukashifu uongozi wa Gavana Nassir kabla ya kumhangaisha na kumfanyia kitendo hicho cha kikatili.

Tayari washukiwa wanne wa kesi hiyo, (Violet Odera, Esther Muthoni, Abdul Hassan na Haji Babu) wamefikishwa Mahakamani na kukanusha mashtaka ya kuhusika, na Mahakama ikiamuru waendelee kuzuiliwa kwa siku 14.

By Mjomba Rashid