LifestyleNewsSiasa

Kigeugeu cha Wabunge wa Mlima Kenya; Wabadili Msimamo wa Kumbandua Gachagua

Baadhi ya Wabunge kutoka eneo la Mlima Kenya ambao waliunga mkono hoja ya kumbandua ofisini Naibu Rais Rigathi Gachagua sasa wamebadili msimamo wao.

Wabunge hao Geofrey Wandeto wa Tetu, Rahab Mukami wa Nyeri na Njoroge Wainaina kutoka bunge la Kieni wamebaini kuwa hawataendelea na juhudi za kumbandua ofisi Gachagua.

Wamedai kuwa baada ya kuskiliza rai za wananchi wao, kutafakari kwa kina na kuisoma hoja hiyo wametambua kuwa ni suala ambalo Naibu huyo wa rais atakaa chini na Rais William Ruto kulitatua kwa kuwa taifa lina umuhimu kuliko kitu kingine.

Kigeugeu hicho cha wabunge hao kinajiri siku moja baada ya majina yao kusomwa bungeni wakiwa miongoni mwa waliotia saini na kuidhinisha hoja ya kumtema nje Gachagua.

Ikumbukwe kuwa wabunge hawa wanatokea katika kaunti ya Nyeri ambako ni ngome ya Naibu rais, na sasa wakisisitiza kuwa mazungumzo ndiyo yanayohitajika kuleta suluhu la mgogoro uliopo baina ya viongozi hao wakuu.

By Mjomba Rashid