Gavana wa Wajir Ahmed Abdullahi amechaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa Baraza la Magavana (CoG).
Hii ni baada ya mkutano wa faragha uliodumu kwa zaidi ya saa tano kati ya magavana wote 47 kabla ya kuamua kwa pamoja kufanya mabadiliko ya mzunguko wa uongozi kati ya muungano wa Kenya Kwanza na Azimio.
Kuchaguliwa kwake Gavana Abdullahi kutoka mrengo wa Azimio kunasisitiza kujitolea kwa Baraza hilo katika kudumisha usawa wa mamlaka na kukuza maelewano kati ya miungano miwili mikuu ya kisiasa.
Wakati uo huo gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga naye ameteuliwa kuwa Naibu Mwenyekiti wa Baraza hilo la Magavana.
Chini ya uongozi wa Mwenyekiti wake mpya na naibu wake, Baraza la Magavana linatarajiwa kupata nguvu na mweleko mpya na kuimarisha mikakati yake.
Itakumbukwa kuwa Abdullahi ambaye alikuwa Naibu Mwenyekiti wa Baraza hilo sasa anachukua uongozi wa baraza hilo kutoka kwa kwa Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru ambaye amehudumu katika wadhfa huo kwa mihula miwili.
BY MJOMBA RASHID