HabariNews

Bunge la Seneti Kujadili na Kuamua Hatma ya Naibu wa Rais

Bunge lote la Seneti sasa litaamua hatma ya Naibu wa Rais Rigathi Gachagua wiki ijayo.

Hii ni baada ya maseneta kupinga suala la kuunda kamati ya watu 11 kujadili hoja ya kumbandua Naibu rais wakisema ni kutokana na uzito wa suala hilo kwa umma.

Kufuatia notisi rasmi iliyotolewa kwa mujibu wa kifungu 145 cha Katiba na Kanuni za Bunge la Seneti, bunge hilo limekutana Jumatano Oktoba 9, kuangazia mashtaka katika pendekezo la kumtimua afisini Naibu wa Rais Rigathi Gachagua.

Spika wa bunge hilo la Seneti Amason Jeffwa Kingi ameafiki uamuzi wa kuruhusu bunge lote kujadili hatma ya Naibu wa Rais, na kuamua vikao hivyo kufanyika Jumatano na Alhamisi juma lijalo ambapo maseneta watakuwa na fursa ya kuchunguza ukweli uliowasilishwa na Bunge la Kitaifa baada ya kuafiki kuwa Gachagua hapaswi kuhudumu kama Naibu wa Rais.

Awali Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Seneti Aaron Cheruiyot aliibua hoja ya kutaka kuundwa kwa kamati ya watu 11 kuchunguza madai hayo na kujadili, hoja ambayo imepingwa huku Seneta Nairobi Edwin Sifuna aliyechaguliwa na Cheruiyot kumuunga mkono, akikataa kuunga hoja hiyo, akitaka bunge lote lishiriki katika vikao vya kujadili hoja hiyo.

Ahsante Mhe. Spika kama ulivyosema awali kuwa hili ni suala ambalo ni la kipekee na limepelekea na kuhitajia kuangaziwa kwa umma kufahamu, na kwa hali ilivyo ya Bunge mimi kwa heshima nakataa kuunga hoja hiyo (ya kuunda kamati).” Alisema.

Hatma ya Gachagua sasa inasalia mikononi mwa maseneta, na iwapo kwa uchache, thuluthi mbili ya Maseneta watashikilia kuunga mkono hoja ya kumbandua, Naibu huyo wa Rais atatimuliwa rasmi afisini.

BY MJOMBA RASHID