HabariNews

Viwango vya mapato visivyo na uhalisia ndicho chanzo cha kudorora kwa maendeleo Kilifi

Ukosefu wa kufikia viwango vya ukusanyaji mapato vinavyowekwa na serikali ya kaunti ya Kilifi kumetajwa kuwa chanzo kikuu cha kudorora kwa maendeleo.

Serikali ya kaunti ya Kilifi inadaiwa kushindwa kutekeleza miradi ya maendeleo inayoazimia kutokana na kuweka viwango vya juu vya mapato inayotaka kukusanya visivyo na uhalisia bila kuweka mikakati mwafaka inayoweza kuepusha kufeli kupata viwango hivyo vya mapato.

Mwanase Ahmed mwanaharakati wa shirika la Uadilifu Kilifi, anasema mfumko katika bajeti inayopendekezwa na serikali ya kaunti ya Kilifi inazidisha changamoto katika kufanikisha miradi iliyo kwenye bajeti za serikali.

Aidha amesisitiza kuwepo ugumu wa kufadhili bajeti inayoanza kwa mapungufu ya mabilioni ya pesa.

“Kwanza kabisa bajeti yetu ina viwango vya juu kupita kiasi vya mfumko na hata ukiangalia mzunguko wa bajeti ya mwaka huu wa kifedha, mapendekezo yetu ya mpango wa maendeleo kila mwaka (ADP) kuna mapungufu ya bajeti ya takriban shilingi bilioni 27. Na kwa yeyote ambaye ni mtaalamu katika maswala ya fedha anajua wazi huwezi ukaanza bajeti ukiwa na mapungufu ya shilingi bilioni 27 kwasababu hakuna vile mtu unaweza ukatimiza malengo yako unahitaji kitu cha uhalisia.” alisema Bi. Ahmed.

Eunice Odhiambo mkaazi mjini Kilifi anasema serikali kutoziba mianya ya kuendeleza ufisadi kwenye ukusanyaji mapato kumechangia serikali kufeli kufikisha kiwango cha mapato inayolenga kukusanya.

Anaeleza kuwa licha ya kuwapo kwa mpango wa maendeleo wa mwaka, baadhi ya miradi ya maendeleo imekwama ama kutotekelezwa, ukosefu wa huduma bora kwa wakazi ukishuhudiwa kaunti ya Kilifi kutokana na kufujwa kwa mapato yanayokusanywa.

“Lakini sasa inasikitisha kuona kuwa kuna mikakati. Na katika awamu ya kwanza ya ugatuzi tuliona. Ukilinganisha ukusanyaji mapato wakati ule wa baraza la mji na wakati wa serikali ya kaunti tuliona tofauti kubwa. Mapato yaliyokusanywa wakati wa serikali ya kaunti ni mkubwa na niwakuridhisha.  

“Lakini nahisi ulifika wakati wale wanaokusanya mapato wakagundua mbinu ya kuiba ama kufuja, yaani kukawa na mbinu ambapo zile pesa zikawa zinafujwa na mpaka kufikia sasa ukusanyaji way ale mapato hauridhishi. Na ikiwa hairidhishi inamaana kuwa ile mipango ya kimaendeleo tuliyonayo kama kaunti hazifanikiwi.” alisema Bi. Odhiambo.

Ikumbukwe ripoti ya utafiti wa bajeti ya kaunti ya Kilifi uliofanywa na shirika la kutetea haki za binadamu KHRC 2024 imeonesha kuwa serikali ya kaunti ya Kilifi imeshindwa kufikia viwango inavyoweka katika ukusanyaji wa mapato, katika mwaka wa kifedha 2021/22, ambapo iliazimia kukusanya shilingi bilioni 1.1 na kufanikiwa kukusanya shilingi milioni 827 pekee ikiwa asilimia 75, mnamo mwaka wa kifedha wa 2022/23, serikali ililenga kukusanya shilingi bilioni 1 na kukusanya shilingi milioni 661 pekee ikiwa ni asilimia 63 huku katika kipindi cha miezi 9 kwenye mwaka wa kifedha wa 2023/24 serikali ya kaunti ya Kilifi ikifanikiwa kukusanya shilingi milioni 554 ikiwa ni asilimia 34.

Erickson Kadzeha