Wanasiasa watatu kutoka kaunti ya Tana River wamefikishwa mbele ya Tume ya Kitaifa ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa (NCIC) kuhusiana na mapigano ya kikabila yanayoendelea katika kaunti hiyo ya Pwani.
Watatu hao ni pamoja na aliyekuwa Mwakilishi wa Wanawake Rehema Hassan, Mbunge wa Galole, Hiribe Said Buya na Mwakiklishi Wadi wa Bangale Jibril Mahamud, ambao walikuwa wameitwa na kueleza NCIC kuhusu mapigano hayo na wanatarajiwa kutoa mwanga zaidi kuhusiana na mapigano makali yaliyohusisha koo mbili za makabila katika vijiji 12.
Kamishna wa NCIC Danvas Makori amesema viongozi hao watasaidia tume hiyo kubaini msingi na chanzo cha mzozo ambao hadi sasa umegharimu maisha ya takriban 14.
NCIC ilikuwa imewaita viongozi watano kuhusu suala hilo akiwemo Mbunge wa Bura Yakub Adow Kuno ambaye kupitia kwa wakili wake ametuma ujumbe kwamba amelazwa hospitalini huku mbunge wa kaunti hiyo Amina Dika Abudulahi akiwasilisha ujumbe kupitia kwa wakili wake kuwa yuko nje ya nchi.
Ijumaa iliyopita, timu ya DCI iliwahoji baadhi ya wanasiasa kutoka kaunti hiyo wakiongozwa na Gavana Godana Dhado kuhusu mapigano hayo.
Ikumbukwe kuwa mnamo Ijumaa wiki jana Waziri wa Usalama wa Ndani Prof. Kithure Kindiki kupitia notisi ya gazeti la serikali alitangaza kaunti ndogo mbili za Tana River kama maeneo hatarishi kwa muda wa siku 30.
By Mjomba Rashid