HabariNews

Pigo kwa Gachagua Mahakama Yakataa Kuzuia Seneti Kusikiliza Hoja ya Kumbandua Afisini

Naibu wa Rais Rigathi Gachagua amepata pigo jingine baada ya Mahakama Kuu kukataa kuzuia Bunge la Seneti kusikiliza hoja ya kumbandua ofisini.

Katika uamuzi wake Jaji wa Mahakama Kuu ya Milimani Chacha Mwita amesema mchakato huo wa kumbandua Gachagua afisini unapaswa kuruhusiwa kuendelea hadi mwishoni.

Uamuzi huo unamaanisha kuwa Bunge la Seneti litaendeleza vikao vya kusikiliza hoja ya kumbandua ofisini Naibu Rais kesho Jumatano na Alhamisi.

Gachagua sasa atajitetea dhidi ya madai yaliyowaslishwa katika Bunge hilo kuhusu kubanduliwa kwake afisini.

Aidha Jaji Mwita ameelekeza suala hilo kwa Jaji Mkuu Martha Koome kuteua jopo la majaji watatu kusikiliza na kuamua kesi hiyo.

Kulingana na jaji Mwita, sasa itakuwa ni juu ya uamuzi wa Jaji Mkuu kulitwika jopo la majaji watatu aliowateua kusikiliza maombi mengine yanayohusu kuondolewa kwa Gachagua afisini na pia kusikiliza ombi la kutaka Seneti isiendelee na kesi hiyo.

By Mjomba Rashid