Naibu Rais aliyebanduliwa afisini Rigathi Gachagua amepata pigo jingine baada ya Mahakama Kuu kushikilia uamuzi wa Naibu Jaji Mkuu kuteua jopo la majaji watatu kuendesha vikao vya kesi yake.
Majaji wa hiyo ya Milimani jijini Nairobi wameamua kuwa Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu anaweza kuwateua majaji wakati wowote anapotekeleza masuala ya utawala na hasa ambapo Jaji Mkuu ikiwa hajaibua pingamizi yoyote.
Wamesema jukumu la Mwilu kama msaidizi wa Jaji Mkuu Martha Koome lilikuwa la kiutawala.
Jopo hilo la majaji watatu linalojumuisha jaji Eric Ogola, Fredah Mugambi na Antony Mrima limesema kuwa Katiba ilikuwa imeainisha wazi majukumu ya Naibu Jaji Mkuu ambayo yalijumuisha kushikilia kwa muda majukumu ya Jaji Mkuu inapohitajika.
Na kuhusiana na uamuzi wa iwapo jopo hilo lilikutana katika nyakati zisizofaa na pasi uwepo wa pande husika katika kesi, mahakama imelitupia mbali ombi hilo ikisema kuwa kikao hicho kilifanyia kisheria.
Mawakili wa Gachagua walikuwa wamedai kuwa jopo hilo la majaji lilifaa kubuniwa na Jaji Mkuu pekee suala lililopingwa na mawakili wa washtakiwa wa kesi hiyo.
By Mjomba Rashid