Naibu Rais aliyetimuliwa afisini Rigathi Gachagua amewasilisha rufaa katika mahakama ya rufaa akisema hajaridhishwa na uamuzi uliotolewa wiki jana na jopo la majaji watatu.
Gachagua anasema kuwa uamuzi kwamba Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu alikuwa na mamlaka ya kuunda jopo hilo la majaji si sahihi, ni potofu na ulizingatia uchanganuzi mbovu wa katiba.
Naibu huyo wa Rais aliyebanduliwa sasa anaitaka Mahakama ya Rufaa sasa anaitaka Mahakama ya rufaa kusitisha shughuli za Mahakama Kuu ikisubiri kusikilizwa na kuamuliwa kwa ombi hilo.
Kupitia mawakili wake Gachagua aidha anadai kuwa majaji wa Mahakama kuu walikataa kurefusha maagizo yaliyotolewa kwa niaba yake akisema ni licha ya juhudi zake na maombi kwa njia ya mdomo kutaka maagizo hayo ya muda yaongezwe.
Majaji watatu wa mahakama hiyo Freda Mugambi, Antony Mrima na Erick Ogola mnamo Jumatano wiki jana waliamua kuwa jukumu la Naibu Jaji Mkuu Philomena Mwilu kama msaidizi wa Jaji Mkuu Martha Koome lilikuwa la kiutawala.
Jopo hilo la majaji watatu lilisema kuwa Katiba ilikuwa imebaini wazi majukumu ya Naibu Jaji Mkuu ambayo yalijumuisha pia kushikilia kama mbadala wa Jaji Mkuu pale inapohitajika.
By Mjomba Rashid