Kikosi kipya cha maafisa wa polisi 600 wa Kenya kitakachotumwa nchini Haiti kuyakabili magenge ya wahalifu kimehitimu tayari kutumwa nchini humo mwezi huu.
Maafisa wa kitengo cha kukabili wizi na kitengo cha kukabili ghasia wameratibiwa kutumwa katika misheni hiyo ya kimataifa ya msaada wa kurejesha usalama kwenye taifa hilo la visiwa vya Carribean.
Wakati uo huo takriban mataifa 10 yameahidi kutuma jumla ya maafisa 2,900 kushirikiana na polisi wa Kenya kuyakabili magenge hayo ya uhalifu.
Tayari Baraza la Umoja wa Mataifa (UN) limeidhinisha kuongezwa kwa muda wa operesheni hiyo kwa mwaka mwingine.
Haya yanajiri huku Rais William Ruto akimpigia simu Rais Mteule wa Marekani Donald Trump na kumweleza kuhusu misheni hiyo ya Kimataifa ya Msaada wa Kiusalama inayoongozwa na vikosi vya Polisi wa Kenya.
Itakumbukwa kwamba ati ati inakumba misheni hiyo hasa kufuatia kuchaguliwa kwa Trump na kwamba huenda akafutilia mbali misheni hiyo inayoungwa mkono na mtangulizi wake Rais anayeondoka Joe Biden ambaye aliahidi shilingi bilioni 38.5.
By News Desk