HabariNews

Mtu Mmoja Afariki, Wanne wakiokolewa katika Jumba lililoporomoka eneo la Majengo-Sega, Mombasa

Mtu mmoja amefariki na wengine wanne wakiokolewa baada ya kufunikwa na mchanga katika jumba linalojengwa eneo la Majengo-Sega, kaunti ya Mombasa.

Kulingana na Waziri wa uchukuzi na Miundomsingi kaunti ya Mombasa na anayesimamia suala la Majanga, Dan Manyala watu watano walikuwa katika eneo la tukio wakiendeleza ujenzi kabla ya kufunikwa na mchanga Jumatatu adhuhuri.

Alisema timu ya uokozi ilifika kwa haraka na kufanikiwa kuwaokoa wanne ambao walikimbizwa hospitali Kuu ya Rufaa na Mafunzo Ukanda wa Pwani, (Makadara) kwa matibabu huku mwili wa aliyefariki ukipelekwa katika hifadhi ya maiti ya Hospitali hiyo.

Waziri Manyala katika eneo la tukio

Tulipata habari kuwa kuna jengo liliokuwa likijengwa na kuna watu waliokuw wamefunikwa na mchanga. Tulituma timu yetu ya uokozi wakafika site na kuanza oparesheni wakisaidiwa na majirani hapa wakaweza kuwaokoa watu wanne pekee kwa bahati mbaya mtu wa tano tumempoteza na tunatoa rambirambi zetu.” Alisema.

Waziri huyo alisema kuwa eneo hilo la ujenzi imefungwa kwa sasa huku timu ya uchunguzi ikishirikisha maafisa wa Idara ya upelelezi DCI na vitengo mbalimbali ikianzisha uchunguzi kubaini kiini cha kisa hicho, sawia na sehemu nyinginezo za ujenzi ili kutathmini na kubaini mikakati ya usalama.

“Tumechukua hatua kufunga site kwa muda, kuna timu zote zimekuja hapa kuna DCI kuna ya Crime scene na tumekubaliana hii site tutaichunguza na kushirikiana na mwekezaji kuhakikisha kisa kama hiki hakitokei tena si hapa pekee bali katika sites zote za ujenzi Mombasa Mombasa county. Kwa sasa tumeifunga uchunguzi unaendelea kujua chanzo cha ajali hii.”

Wakati uo huo Manyala alisema wameagiza wakazi walio karibu na jumba lililoporomoka kuhamia eneo jingine kutokana na athari na nyufa zilizojitokeza baada ya tukio hilo.

Tuna hofu sana msingi wa hii nyumba karibu hapa labda imeathirika kwa hii kisa, tunaona kuna mporomoko mkubwa na tuna hofu kubwa so tumetoa maagizo kwa maafisa wetu kutathmini na kuchunguza nyumba ile iko salama kwa wakazi pale lakini kwa sasa wakazi pale waondoke kwa muda ili tuangalie usalama wao.”

By Mjomba Rashid