HabariNews

Magavana Kusitisha Huduma katika Kaunti iwapo Mgao wa Fedha Hautasambazwa kwa haraka

Baraza la Magavana CoG, limetishia kusitisha kutoa huduma katika kaunti zote 47 nchini iwapo Serikali Kuu haitakuwa imetoa fedha za kaunti zilizosalia.

Baraza hilo limesema kaunti nyingi zimelazimika kupunguza bajeti yake huku baadhi ya wafanyakazi wakikosa malipo yao kwa zaidi ya miezi mitatu sasa.

Mwenyekiti wa Baraza hilo Ahmed Abdullahi amesema Wizara ya fedha bado haijawasilisha shilingi bilioni 63.8 za kuanzia Mwezi Septemba, akionya kuwa kufikia mwisho wa mwezi huu Novemba kaunti zitakuwa hazina fedha zozote.

Akihutubia wanahabari jijini Nairobi, Abdullahi ambaye pia ni Gavana wa Wajir amesema kwa sasa kaunti zinatumia asilimia 50 ya mgao iliyosambazwa mwaka jana na mpango huu utakamilika Disemba mwaka huu na kuiacha kaunti katika hatari ya upungufu kamili wa fedha kufikia Januari mwakani.

Aidha Abdullahi amesema si haki kwa shughuli kuendelea kama kawaida serikali kuu huku shughuli za kaunti zikilemaa, akisema bajeti ya ziada inayopendekezwa ni kinyume cha katiba na kutilia shaka mchakato huo.

Na kuhusu bima ya afya ya jamii SHA amesema hospitali za umma bado hazijapokea shilingi bilioni 9.1.

Wakati huo huo Magavana wameibua wasiwasi kucheleweshwa kwa kupitishwa kwa mswada wa ugavi wa mapato ya kaunti ambao bado haujaidhinishwa licha ya kupitishwa na Bunge la Kitaifa miezi 5 iliyopita.

Amewapongeza maseneta kwa kuhsikilia mgao wa fedha kusalia bilioni 400 huku akilitaka Bunge la Seneti kupitisha mswada wa ugavi wa mapato ili kusaidia kucheleweshwa mgao wa fedha.

By Mjomba Rashid