Suala la ushuru wa juu zaidi unaolengwa kutozwa wafanyabiashara katika mswada mpya wa fedha limetamalaki katika kikao cha kukusanya maoni ya umma kuhusu mswada huo.
Wakazi wa kaunti ya Mombasa wameelezea kutoridhishwa kwao na baadhi ya vipengee vya marekebisho ya miswada 6 ikiwemo Sheria za biashara, Taratibu za ushuru na Sheria za Kodi 2024, vinavyolenga kuongeza ushuru zaidi kwa Wakenya.
Katika kikao hicho cha kukusanya maoni kuhusu marekebisho ya miswada 6, kilichoandaliwa na Kamati ya Fedha na Mipango katika Bunge la Kitaifa mjini Mombasa, wakaazi waliojitokeza kutoa maoni yao wamelalamikia kodi ya wafanyabiashara ikizingatiwa kuwa imezidi hata ile ya wafanyabiashara waliotoka mataifa ya kigeni na kuwekeza nchini.
“Bei ya vyakula imepanda, mambo yalivyo sasa naona mmeongeza ushuru kuanzia sh. 360,000 na kabla sijastaafu tax free ilikuwa kuanzia 240,000 ila hali ilivyo sasa na uchumi katika nchi yetu naomba ushuru uanze kuanzia nusu milioni taxation ianzia hapo.” Alisema mkazi mmoja wa Mombasa.
Aidha wamesema iwapo vipengee hivyo vitapitishwa vitaongeza mzigo zaidi kwa mwananchi wa kawaida sawia na kuwafukuza wawekezaji ambao huajiri Wakenya.
“Naomba wabunge wetu muangalie vile wawekezaji wanaweza kuja kenya, mkieka kiwango cha juu sana wawekazaji watakosekana kwa sababu wakija hapa matajiri 10 wataajiri watu hata elfu moja mbili na zaidi, ile kodi mnataka itapatikana.” Akasema mmoja.
Wakati uo huo wameisuta kamati hiyo wakisema licha ya awali kuendesha zoezi hilo, imekuwa ikipuuza maoni ya wakenya na kutekeleza sheria zinazomkandamiza mkenya wa kawaida kinyume na matakwa na mapendekezo yake.
Wakaazi wa Mombasa aidha wamelalamikia matumizi ya lugha ngumu kwenye mswada huo ambayo ni ngumu kueleweka kwa urahisi na kila mkenya.
“Mmetwambia lugha itatumika hapa ni Kiswahili na Kiingereza hizi document zimeletwa hapa lugha ni very technical, ili mpata jawabau ya kisawaswa n ngumu. Kisha mnatuambia ni amendments (marakebisho) marekebisho ni kurekebisha kutokana na kitu na hicho kitu hatukioni hapa,” akasema.
Kamati ya Fedha na Mipango katika katika Bunge la kitaifa inayoongozwa na Mwenyekiti wake Kimani Kuria imekuwa na wakati mgumu kuelezea baadhi ya vipengee tatanishi ambavyo vilipata pingamizi kali kutoka kwa wakaazi wa Mombasa.
Hata hivyo Mwenyekiti huyo amebaini kuwa maoni yao hayo yatajumuishwa na kutekelezwa ipasavyo, huku akitoa wotp kwa vijana kushiriki katika vikao sawia ili kupaza sauti zao.
“Kama ule mswada ambao uliweza kuleta vurugu katika nchi yet, maswala yote ambayo wananchi walisema hawayataki kamati hii iliweza kuitoa kwenye ripoti yetu, na katika vipengele vilipitishwa bunge hayo maswala yote ambayo yaliweza kuwakera Wakenya yote yalikuwa yametolewa; kwa hivyo si kweli kwamba hatusikilizi Wakenya.” Alisema Kimani.
By Mjomba Rashid