HabariNews

Mzozo wa Ugavi wa Raslimali za Kaunti Watatuliwa; Kaunti kupata nyongeza ya shilngi bilioni 2

Hatimaye Bunge limefanikiwa kupata suluhu la ugavi wa raslimali suala ambalo limekuwa likiibua mvutano kuhusu kiwango cha kinachopaswa kusambazwa kwa serikali za kaunti nchini.

Serikali za kaunti sasa zinatarajiwa kupokea shilingi bilioni 387, hii ikimaanisha kuwa zitapokea shilingi bilioni 2 zaidi ya zile ilizopokea mwaka uliopita.

Ndidi Nyoro ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti katika Bunge la Kitaifa na anasema Kamati ya Maridhiano ya Seneti na Bunge la Kitaifa kuhusu Mgao wa Raslimali imeafikiana kwa kauli moja kuwa kaunti zinahitaji raslimali zaidi.

Hatuwezi kuruhusu kuzipa kaunti zetu fedha chache kuliko walizopokea mwaka wa kifedha uliopita. Tumeamua kwa pamoja kuwa kaunti zetu zinahitaji raslimali za kutosha na kwa sababu hiyo tumeongeza kiwango walichopata mwaka uliopita kutoka bilioni 385 na juu yake tumwaongezea shilingi bilioni 2 kuzifanya kaunti zetu zitekeleze wajibu wake vilivyo.” Alisema Nyoro.

Baada ya vuta nikuvute ya awali, kikao cha maridhiano na upatanisho kati ya seneti na bunge la Kitaifa, hatimaye kamati zimeafikiana kiwango hicho licha ya kaunti awali kushinikiza mgao wa shilingi bilioni 400.

Ali Roba Ni mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti katika Bunge la Seneti na anaeleza kuwa licha ya kushinikiza mgao zaidi kwa kaunti, athari za kutupiliwa mbali kwa mswada wa fedha 2024 zimekuwa kikwazo kwa kila idara.

By Mjomba Rashid