HabariNews

Mahakama Yasitisha Agizo la Serikali la Kuwataka Abiria wanaokuja Kenya kutangaza Nambari za IMEI za simu

Mahakama Kuu imesitisha maagizo ya Serikali kutekeleza agizo la kuwataka abiria wanaoingia nchini Kenya kuweka wazi nambari za Utambulisho wa Simu (IMEI) za simu zote wanazopania kutumia wakiwa nchini.

Jaji Chacha Mwita ametoa maagizo hayo akisubiri kusikilizwa kwa kesi iliyowasilishwa na Taasisi ya Katiba.

Kwa sasa, hifadhi inatolewa kusimamisha utekelezaji wa notisi iliyotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya tarehe 24 Oktoba 2024 yenye kichwa: “Ilani kwa Umma juu ya kuimarisha uzingatiaji wa ushuru wa Vifaa vya rununu nchini Kenya” pamoja na notisi inayofuata ya mamlaka ya Ushuru ya Kenya. Tarehe 5 Novemba 2024…,” kama inavyosomeka amri ya mahakama.

Mamlaka ya Mawasiliano nchini CA, na ile ya Ukusanyaji Ushuru KRA, zilitoa notisi ya umma mnamo Oktoba 24 na Novemba 5 mtawalia kuhusu uzingatiaji wa ushuru wa vifaa vya rununu kwa kuwataka watu binafsi wanaoingia nchini kutangaza nambari za utambulisho wa Simu, IMEI.

Taasisi ya Katiba mnamo Ijumaa iliwasilisha ombi Mahakamani kupinga agizo jipya la kuwataka abiria wanaoingia nchini kuweka wazi nambari zozote za utambulisho wa simu (IMEI) wanazopania kutumia wakiwa nchini.

Baada ya notisi ya Mamlaka ya Mawasiliano, CA, Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru nchini (KRA) nayo iliwasilisha sera hiyo mnamo Novemba 5, ikisema kuwa hatua hiyo ni sehemu ya mpango wa kuimarisha uzingatiaji wa ushuru.

Katika ombi lake, Taasisi ya Katiba inasema kwamba ufichuzi wa lazima wa nambari za IMEI unaleta hatari kubwa kwa haki za kimsingi za watu binafsi na uhuru wao na kuiwezesha ufuatiliaji wa Serikali usio na msingi.

Taasisi hiyo pia inaibua wasiwasi wa ukosefu wa uwazi kuhusu ulinzi wa data inayokusanywa, ikihoji  ni nani atakayedhibiti na kufikia hifadhidata ya IMEI, na ni hatua zipi za usalama zinazotumika, na kama suluhu madhubuti zitapatikana kwa watu ambao watakuwa hawajaridhika na ukusanyaji wa data hii.

Inapojumuishwa na maelezo ya ziada ya kibinafsi, kama vile majina au maelezo ya ndege na forodha, nambari za IMEI zinaweza kutumika kutambua watu binafsi na hivyo kuunda data ya kibinafsi,” kama lilivyosomeka hilo.

Imeonya kuhusu hatari zinazoweza kutokea za kukusanya nambari za IMEI bila uangalizi mzuri, ikisisitiza udharura wa kusitisha kile inachokitaja kama “mwenendo mbaya.”

Kusitishwa kwa muda maagizo hayo kunatoa afueni kwa abiria wanaoingia nchini ambao wengi wao wameonekana kulalamikia sera hiyo.

Kesi hiyo itasikilizwa mnamo Desemba 18, 2024.

By Mjomba Rashid