Mahakama Kuu imesitisha utekelezaji wa mikataba yote kati ya Serikali na Kampuni ya Adani Group kutoka India.
Jaji wa Mahakama hiyo Bahati Mwamuye ameamuru Kampuni hiyo ya Adani kuzuiwa kuchukua usimamizi na mali za Uwanja wa ndege wa JKIA Nairobi.
Jaji Mwamuye aidha ameiagiza Serikali kuwasilisha ushahidi mahakamani kuthibitisha uamuzi wa Rais William Ruto kufutilia mbali mikataba na Kampuni ya Adani kufikia Januari 25 mwakani.
Wakati huo huo Mahakama hiyo imetoa amri za kuzuia serikali ya Kenya kuingia katika mikataba zaidi na Kampuni hiyo kubwa ya kimataifa ya Adani.
Hata hivyo kampuni ya Adani kupitia wakili wake Ezra Makori imewasilisha ombi la kutolewa katika kesi hiyo ikisema kuwa hakukuwa na mkataba wowote kati ya kampuni hiyo na serikali ambao umekamilika na hivyo hakuna kitu cha kusitishwa.
Kulingana na mawakili wa Adani, mikataba na serikali ilikuwa bado katika hatua za awali, na hakuna mkataba wa kisheria uliotiwa saini.
Kesi hiyo imeratibiwa kusikilizwa tena Januari mwaka 2025.
Wakati uo huo Timu ya mawakili kutoka mrengo wa Upinzani ikiongozwa na Wakili tajika aliye pia Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka, ikiwa miongoni mwa waliowasilisha kesi mahakamani kuhakiki mchakato wa kuondolewa kwa Adani.
Akizungumza nje ya majengo ya Mahakama Kuu ya Milimani Kalonzo amesisitiza kuwa mikataba iliyositishwa na Serikali ni sharti iwasilishwe mahakamani kama ushahidi na uthibitisho wa kusitishwa kwayo.
Wakati uo huo Kalonzo ametaka kuwekwa bayana maelezo ya ziada kuhusu maafisa wa Kenya aliodai kupokea kiwango kikubwa cha malipo, hasa ikizingatiwa kuwa wanakabiliana na kesi ya ufisadi wa hali ya juu ambayo imeathiri hadi mataifa mengine ulimwenguni.
Kalonzo amewahakikishia Wakenya kuwa watafuatilia suala hilo hadi ukomo wake.
By Mjomba Rashid