Muungano wa madaktari nchini (KMPDU) umeagiza madaktari wanagenzi kusitisha kazi katika hatua ya kupaza lalama zao kufuatia kifo cha mmoja wao Dkt. Francis Njuki aliyeripotiwa kujiua kutokana na shinikizo kazini.
Kulingana na Katibu mkuu wa KMPDU Dkt. Davji Atellah wengi wa madaktari wanagenzi hawawezi kuendelea na majukumu yao kutokana na serikali kushindwa kulipa malipo yao jambo linalowafanya baadhi yao kugeukia kujitoa uhai.
Amesema ndani ya mwezi mmoja madaktari wawili wanagenzi wamejitoa uhai huku wengine watano wakiokolewa baada ya majaribio ya kujitoa uhai kutokana na shinikizo za kazi na kukosa malipo.
Dkt. Atellah sasa anasema kuwa chama hicho cha madaktari kitaandaa mgomo mkubwa kabla ya mwisho wa mwaka baada ya serikali kushindwa kutekeleza na kuheshimu makubaliano ya kurejea kazini ambayo ilitia saini na wao mwishoni mwa mgomo wa siku 56 mapema mwaka huu.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa KMPDU Dkt. Dennis Miskellah ameibu wasiwasi kuhusu uwezekano wa Wakenya zaidi kupoteza maisha iwapo madaktari watashiriki mgomo, hata hivyo akiwasihi Wakenya kuungana nao katika maandamano yao ya mwezi Desemba.
Iwapo madaktari watatekeleza kitisho chao cha kushiriki mgomo taifa litatumbukia kwenye mgomo mwingine wa pili ndani yam waka mmoja na kusababisha mahangaiko zaidi kwa Wakenya wanaoendelea kutatizwa na changamoto za bima mpya ya afya SHA na changamoto za kiuchumi.
By Mjomba Rashid