Wahudumu wa afya wa Muungano wa hospitali za kibinafsi za mijini na pia mashinani RUPH, sasa wanapendekeza kufanyika kwa mazungumzo na serikali ya kaunti ya Mombasa ili kutatua mzozo unaotokota kwa kasi kati yao na serikali hiyo
Wakizungumza na waandishi wa habari hapa mjini Mombasa wahudumu hao wakiongozwa na mwenyekiti wao DR Brian Lishenga walisema serikali ya kaunti ya Mombasa inawatoza ushuru maradufu kinyume cha sheria na sasa wanataka mazungumzo kati yao na serikali ya kaunti kufanyika ili kutatua suintofahamu inayozingira kliniki na kutafuta suluhu la kudumu badala ya vuta ni kuvute na ubabe usiokuwa faida kwa mwananchi wa kawaida .
“ Kwa hivyo sisi tunasema kwanza majadiliano. Wakubali tuongee maana kuna amri iliyoko ya mahakama. Na ikiwa hawatataka kuongea, basi tutachukua mbinu za kisheria dhidi yao.” Alisema DR Lishenga
Aidha walibua madai ya unyanyasaji na dhuluma kutoka kwa maafisa wa kaunti wanaowashurutisha kulipia kibali cha kuendesha huduma katika zahanati zao wakisema hali hiyo imefanya huduma za matibabu kuwa ghali mno kwa mwananchi wa kawaida.
“Hiki Kibali cha kibiashara kina ushuru maradufu. Tayari wanachama wetu wanalipa ushuru mwingi kwa idara husika na zinazofaa kwa mujibu wa sheria na sasa kuleta ushuru mwingine ni hujuma. Hata huduma wanazofaa kupata wananchi hawapati.” Aliongeza Lishenga.
Muungano kadhalika uliiomba serikali ya kaunti ya Mombasa kufuata na kuheshimu amri ukiwataka maafisa wa serikali ya kaunti ya Mombasa maafisa hao kutohujumu sheria na amri iliyotolewa na Mahakama la visivyo wawachukulie hatua kazi za kisheria.
“Ikiwa kaunti ya mombasa itaendelea kudhulumu wahudumu hawa basi itabidi tuwachukulie hatua maafisa husika wanaotumika kutekeleza hila hiyo. Wewe kama afisa wa kaunti utaingia katika hospitali ya kibinafsi na hudhulumu ama hubebe mitambo na tujue kitambulisho chako, au utambuliwe wewe tutakuchukulia hatua kali za kisheria.” Alisema Lishenga
Kauli ya wanachama wa muungano huo inajiri huku madai yakiibuliwa kwamba serikali ya kaunti ya Mombasa inawatoza ushuru maradufu kinyume cha sheria na pia amri ya mahakama ya 2021 inayozizuia kaunti zote kutoza ushuru wanachama wa muungano huo.
BY ISAIAH MUTHENGI