HabariNews

Watu wawili Wakamatwa wakisambaza dawa ghushi za kuua Wadudu Kilifi

Maafisa wa Bodi ya Dawa za Wadudu (PCPB) wakishirikiana na Maafisa wa Idara ya Upelezi DCI, wamewakamata washukiwa wawili waliokuwa wakisambaza dawa ghushi za kuua wadudu kaunti Kilifi.

Washukiwa hao walikamatwa maeneo ya Mtondia walipokuwa wakisambaza dawa hizo.

Akiongea wanahabari Afisa Mwandamizi wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa sheria katika Bodi hiyo eneo la Pwani Shaban Karisa alisema kwamba washukiwa hao walinaswa na dawa hizo ghushi kilo 200 zenye thamani ya shilingi 400,000.

Afisa huyo hata hivyo amewatahadharisha wananchi kuwa makini, akiwataka kutoka kwa maduka yaliyokaguliwa na kupewa leseni na bodi ya PCPB kwani dawa ghushi na zile ambazo hazijasajiliwa ni hatari kwa afya ya binadamu na mazingira.

“Tungependa kutahadharisha wananchi waende kwa maduka yaliyoidhinishwa kuuza dawa za sumu au kuua wadudu, wasiende kununua kwa maduka ya kawaida, ni hatari sana.” Alisema.

Oparesheni na msako dhidi ya wauzaji dawa ghushi unaendelezwa katika kaunti nyingine za eneo la Pwani, onyo likitolewa kwa wachuuzi na wauzaji dawa za sumu ambao hawajaidhinishwa kuwa watakabiliwa kisheria.

By Mjomba Rashid