HabariNews

Utafiti wa Infotrack Wabaini Wakenya wengi Hawana Imani na IEBC kuendesha Uchaguzi Huru na Haki 2027

Asilimia 54 ya Wakenya sasa haiamini kuwa Tume huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC itaendesha uchaguzi huru na wa haki mwaka 2027.

Hii ni kulingana na Kura ya maoni ya hivi punde ya Infotrak ambayo imefichua kuwa ni aslimia 26 pekee ndiyo ina imani na tume hiyo kuwa mawakala wa IEBC wataendesha uchaguzi wa uwazi, huru na haki.

Ripoti hiyo ya utafiti iliyotolewa Jumatatu Desemba 16, inaonesha kuwa kiwango cha imani cha Wakenya kwa IEBC kinakatisha tamaa, huku idadi kubwa ya waliotilia shaka uwezo wa IEBC kuandaa uchaguzi wa kuaminika wakitoka eneo la Mashariki mwa Kenya, Kaskazini Mashariki, eneo la Kati, Magharibi, Nyanza na Bonde la Ufa.

Akiwasilisha matokeo ya utafiti huo uliofanywa kati ya Novemba 16 na 30, Mkurugenzi Mtendaji wa Infotrak Angela Ambitho alisema Wakenya waliohojiwa walitaja uingiliaji kutoka nje kama wasiwasi wao mkuu, kwa asilimia 39.

Kura hiyo ya maoni pia imebaini  kuwa asilimia 38 ya Wakenya wana fikra kuwa Tume hiyo haitaitafanya kazi kutokana na ufisadi, huku asilimia 38 wakiona ukosefu wa makamishna wa IEBC kuwa suala kuu.

Vile vile, kura ya maoni ilifichua kuwa asilimia 41 ya Wakenya hawana vitambulisho, suala ambalo huenda likawazuia kujiandikisha kama wapiga kura.

Wakati huo huo, asilimia 16 ya waliohojiwa walitaja ratiba yenye shughuli nyingi kuwa sababu ya wao kutoshiriki katika uchaguzi mkuu uliopita.

Kura hiyo ya maoni pia ilibaini kuwa asilimia 75 ya Wakenya kote katika mikoa yote hawajahusika katika ushiriki wowote wa umma unaowanyima sauti ya kufanya maamuzi muhimu nchini.

Huku hayo yakijiri, utafiti huo wa Infotrack aidha ulibainisha kuwa asilimia 51 ya Wakenya wana wasiwasi zaidi na gharama ya maisha, asilimia 36 kuhusu ukosefu wa ajira, asilimia 24 kuhusu viwango vya ufisadi nchini na asilimia 23 kuhusu kutozwa ushuru kupita kiasi na kuhama kutoka NHIF hadi SHIF.

By Mjomba Rashid