HabariNews

Baraza la Mawaziri Laidhinisha Mswada wa kutoza faini ya Milioni 10 kwa Maafisa Wanaotatiza Kipindi cha Mpito cha Urais

Baraza la Mawaziri limeidhinisha Mswada mpya unaolenga kushughulikia mianya katika mpito wa mamlaka ya utendaji na kuchukua mamlaka kwa Rais mteule.

Mswada huo wa Kuchukua Ofisi ya Rais na Mpito wa Mamlaka ya Utendaji 2024, unalenga kuziba mapengo na kuhakikisha kuwa kunakuwa na urahisi na umoja zaidi wa mpito wa urais nchini Kenya

Katika Kikao cha Baraza la Mawaziri kilichoongozwa na Rais William Ruto mnamo Jumanne na ambacho ni cha mwisho kwa mwaka huuBaraza hilo liliidhinisha mswada huo unaoleta sheria ya umoja inayohusu kutwaa madaraka kwa Rais Mteule na mpito wa mamlaka ya utendaji.

Mswada huo, ambao sasa unaelekea Bungeni kwa ajili ya kufanyiwa tathmini, unalenga kuhakikisha kuwa Rais mteule na Naibu Rais mteule watapokea mipangilio ya usalama sawia na ya Rais aliye madarakani na Naibu wake.

Mswada huo wa Sheria aidha utatoa adhabu kali kwa maafisa wa Serikali na wa umma ambao watazuia mpito huo, ikipendekeza faini ya hadi shilingi milioni 10, kifungo cha hadi miaka 10, au vyote kwa pamoja.

Katika hali ambapo rais anayeondoka mamlakani hataweza kuhudhuria sherehe ya kuapishwa na hata kukabidhi vifaa vya mamlaka kama vile upanga na kitara, mchakato wa kukabidhi vifaa vya mamlaka utaachwa bila kuathiri uhalali wa utaratibu mzima wa mpito na mchakato wa kuapisha Rais mteule.

Sheria inayopendekezwa pia inahakikisha mwendelezo wa shughuli za serikali kwa kuruhusu Mawaziri na Makatibu Wakuu kusalia ofisini hadi uteuzi mpya utakapofanywa na uongozi unaoingia.

Kulingana na mswada huo, mpito wa mamlaka ya utendaji utakamilika mara tu Rais, Naibu Rais, Mwanasheria Mkuu, Mawaziri, Makatibu na Katibu katika Baraza la Mawaziri watakaposhika madaraka.

Mswada huo pia unaeleza kuanzishwa kwa kituo cha mpito na uteuzi wa wajumbe wa Kamati ya Kuchukua mamlaka ya Ofisi ambao jukumu lao litahusisha kuwezesha mchakato wa kukabidhiwa kwa rais anayeondoka kwa rais mteule.

Mswada huo utaelekea Bungeni ili kuzingatiwa na Mabunge yote mawili.

By Mjomba Rashid