HabariNews

Rais Ruto Akwea Mlima; Awajumuisha Wandani wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta Serikalini

Rais William Ruto mnamo Alhamisi aliwateua wandani wa rais mstaafu Uhuru Kenyatta katika Baraza la Mawaziri.

Juma moja baada ya Rais Ruto kufanya ziara ya ghafla nyumbani kwa rais mstaafu huko Ichaweri eneo la Mlima Kenya na kudai kujadiliana naye suala la kuunganisha taifa na kuepuka migawanyiko, hatimaye ameonekana Katika panga pangua hiyo rais amemteua aliyekuwa Waziri wa Afya katika serikali ya Uhuru Kenyatta, Mutahi Kagwe.

Kagwe aliyegonga vichwa vya habari wakati wa kipindi cha ugonjwa wa Korona atarejea serikalini kuhudumu kama Waziri wa Kilimo na Mifugo.

Iwapo itaidhinishwa na bunge, Mutahi Kagwe atakuwa akichukua mikoba ya wizara kutoka kwa Dkt. Andrew Karanja ambaye ndiye Waziri wa sasa wa Kilimo na Maendeleo ya Mifugo.

Katika kile kilichoonekana kutafuta uungwaji mkono na kurejesha utulivu wa kisiasa eneo la Mlima Kenya hasa baada ya kubanduliwa kwa aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua, rais alimteua Gavana wa zamani wa Nakuru Lee Kinyanjui kuwa Waziri wa Biashara na Viwanda, vilevile akimpendekeza aliyekuwa gavana wa Kiambu William Kabogo kushikilia Wizara ya Habari na Mawasiliano, ICT.

Rais aidha alifanya mageuzi katika wizara kadhaa kwa kumhamisha Salim Mvurya kutoka wizara ya biashara hadi ya Michezo na Vijana, naye Kipchumba Murkomen akihamishwa katika Wizara muhimu ya masuala ya Kitaifa na Usalama wa Ndani.

Katika taarifa iliyotolewa mapema Alhamisi jioni na Mkuu wa utumishi wa umma Felix Koskei, Rais Ruto aidha alimteua aliyekuwa waziri wa michezo Ababu Namwamba kuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Kenya katika Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Mazingira, UNEP afisi za Nairobi, huku Dkt. Andrew Karanja ambaye ni waziri wa Kilimo kwa sasa akihamishwa na kuteuliwa kuwa Balozi wa Kenya nchini Brazil.

By Mjomba Rashid