Idara ya mahakama nchini imekashifu visa vya hivi punde vya kutekwa nyara kwa raia waliohusika katika kumkosoa rais William Ruto na serikali yake kupitia mitandao ya kijamii.
Katika chapisho kwenye mtandao wa kijamii mnamo Alhamisi, mahakama ilisema utekaji nyara unatishia haki za kikatiba za raia wa Kenya na kwamba hauna nafasi kisheria nchini.
“Kenya ni taifa la demokrasia ya kikatiba, ambapo utawala wa sheria unasimama kama thamani ya msingi na kanuni elekezi ya utawala wetu. Utekaji nyara hauna nafasi kisheria na kwa hakika ni tishio la moja kwa moja kwa haki za raia.” Idara ya Mahakama ilisema.
Mahakama aidha ikiitaka idara ya Polisi kuzingatia sheria na katiba ya nchi katika utendakazi wao.
“Kutokana na ripoti hizi, tunahimiza sana mashirika ya usalama na vyombo vyote vilivyounganishwa kuzingatia sheria ili kulinda haki za kimsingi na uhuru,” iliongeza.
Kauli ya Mahamama ikijiri kufuatia kilio na shinikizo za Wakenya kuhusu kutekwa nyara kwa wananchi ambao wameonekana kuikosoa serikali.
Watu hao waliotekwa wametumia maneno ya kisanii ikiwa ni pamoja na katuni za silhouette, picha zinazozalishwa na Akili Mnemba (AI) na jumbe maarufu (memes) kumkosoa Rais William Ruto.
Mapema Alhamisi, Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja alijitokeza kukanusha tuhuma akisema Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS) haihusiki na utekaji nyara na hakuna hata mmoja wa waliotekwa nyara anazuiliwa katika vituo vya polisi.
Aidha Kanja alikashifu umma kwa kile alichokitaja kuwa ni kuiharibia sifa ya Idara ya Polisi nchini, NPS.
Mchoraji katuni Kibet Bull, kakake Rony Kiplangat, Bernard Kavuli, Peter Muteti na Billy Mwangi ni miongoni mwa watumiaji wa mitandao ya kijamii ambao wameripotiwa kutoweka.
By Mjomba Rashid