HabariLifestyleNews

Rais Ruto awateua Mawaziri Mudavadi, Duale na Mvurya wizara za ziada

Rais William Ruto amewaongezea majukumu ya wizara Mawaziri Musalia Mudavadi, Aden Duale na Salim Mvurya kukaimu nyadhfa zilizo wazi katika Baraza la Mawaziri.

Mabadiliko hayo yaliyotangazwa Jumamosi na Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei sasa yatamfanya Mudavadi, ambaye kwa sasa ni Waziri Mkuu na Waziri wa Masuala ya Kigeni, pia kuchukua jukumu la Wizara ya Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Kidijitali.

Aden Duale, ambaye ni Waziri wa Mazingira, Mabadiliko ya Tabianchi na Misitu, naye ametwikwa kukaimu jukumu la Wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Mifugo, huku Salim Mvurya, ambaye anaongoza Wizara ya Michezo na Masuala ya Vijana, akiwa Kaimu Waziri wa Biashara, Uwekezaji na Viwanda.

Majukumu hayo mapya yanafuatia mabadiliko ya Rais Ruto ya mnamo Desemba 19, ambapo Kipchumba Murkomen alihamishwa kutoka wizara ya Michezo na kuteuliwa kuongoza Wizara ya Mambo ya Ndani; Mvurya, aliyekuwa Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda, akichukua nafasi yake.

Rais alimteua aliyekuwa Gavana wa Nakuru Lee Kinyanjui kuchukua wadhifa wa Wizara ya Biashara inayoongozwa na Mvurya, huku Mutahi Kagwe aliyekuwa Waziri wa zamani katika serikali ya Uhuru Kenyatta akiteuliwa katika Wizara ya Kilimo, naye William Kabogo aliteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Mawasiliano na Uchumi wa Dijitali.

Katika taarifa yake kwa vyombo vya habari Koskei amesema rais Ruto amewapa majukumu mawaziri hao watatu kukaimu wizara hizo wakati mawaziri aliowateua awali wakisubiria mchakato hitajika wa ukaguzi na kuidhinishwa na bunge.

Wakati Mawaziri wateule wakipitia mchakato unaohitajika wa kuidhinishwa na bunge, Mheshimiwa Rais amewateua makaimu Makatibu wa Baraza la Mawaziri kwa nyadhifa za mawaziri zilizo wazi,” alisema Koskei katika taarifa kwa vyombo vya habari.

Wabunge wanatazamiwa kuwakagua walioteuliwa na mawaziri mnamo Januari 14, 2025.

By Mjomba Rashid