Viongozi wa mataifa ya Afrika Mashariki wameendelea kumtafutia uungwaji mkono mgombea wa Uenyekiti wa Tume ya Africa, AUC Raila Odinga anapolenga kuchukua kiti hicho.
Akizungumza alipohudhuria Tamasha la Kitamaduni la Piny Luo huko kaunti ya Siaya Rais William Ruto amesisitiza kuwa Odinga ana uwezo wa kuangazia maslahi ya bara la Afrika na kwamba ndiye anayefaa kwa kiti hicho hasa kutokana na tajriba yake kisiasa.
Rais Ruto aidha ameeleza matumaini ya Odinga kunyakua kiti hicho kutokana na uungwaji uungwaji mkono wa viongozi mbalimbali, akisisitiza kuwa Odinga anaweza kuliunganisha bara la Afrika na kuleta mabadiliko mwafaka atakaposhinda wadhfa huo.
“Raila si mgombea wa Kenya, ni mgombea wa Afrika Mashariki, kabla hatujaanza kugombea tulikwenda kwa Mzee Museveni tukazungumza na wakuu wote wa nchi za Afrika Mashariki na kuthibitisha kuwa tuna mgombea anayefaa na mwenye sifa stahiki kupigania umoja, maendeleo na mafanikio ya Afrika,” Ruto alisema.
Rais wa Uganda Yoweri Museveni ameunga mkono azma ya Raila Odinga kunyakua wadhfa wa Uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika katika uchaguzi wake ulioratibiwa kufanyika Februari jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Akizungumza wakati wa tamasha hilo la Piny Luo katika Kaunti ya Siaya, Museveni amemfananisha Odinga na Yohana Mbatizaji katika Biblia, kwa ari na shauku yao ya kuzungumza wanachokiamini.
Ameeleza kuwa itikadi na sera zozote ambazo Raila atakuja nazo zinafaa kuungwa mkono na maafisa wa serikali ili kuunganisha mataifa ya Bara hili na kuhakikisha halitakuwa katika athari ya vitisho vyovyote vya kiusalama na mataifa ya ughaibuni.
“Tunaunga mkono mgombeaji wa Raila kuwa mwenyekiti wa AUC. Atatusaidia kufanya uhamasishaji na mawazo lakini nguvu halisi iko nasi hapa,” Museveni alieleza.
“Wale walio madarakani (maseneta, magavana, wabunge) wanaweza kuamua kuhama au la. Kwake yeye anaweza kuzungumza, yeye ni kama mhubiri, kama Yohana Mbatizaji.”
Wakati uo huo Museveni ameangazia muungano wa kisiasa na maendeleo ya mataifa ya Afrika akiwataka viongozi wa bara hili kushughulikia mbinu mwafaka za kibiashara kujiimarisha pasi kutegemea misaada ya mataifa ya nje.
Kwa upande wake Mgombea wa Uenyekiti wa AUC, Raila Odinga amesisitiza haja ya kuunganisha Waafrika wote akisema njia mojawapo ya kuwaunganisha wakazi wa bara hili ni kupitia biashara.
Amesisitiza haja ya mataifa ya Afrika kufungua mipaka yao kwa wananchi wa bara hili akisema mataifa ya nje ya bara hili yamekuwa yakinufaika na biashara kutoka hapa Afrika kuliko mataifa yenyewe yaliyo hapa Afrika.
By Mjomba Rashid