Gavana wa Mombasa Abdulswamad Shariff Nassir amepinga mfumo mpya wa ugavi wa fedha kwa serikali za kaunti unaopendekezwa na Tume ya Ugavi wa Mapato kwa kaunti, CRA.
Mfumo huo mpya uliopendekezwa na CRA unapendekeza mgao wa shilingi bilioni 417 kwa Kila kaunti huku kaunti zenye idadi kubwa ya watu zikipendekezwa kupokea mgao mkubwa wa fedha.
Gavana Nassir ameyakosoa mapendekezo ya mfumo huo mpya wa ugavi wa mapato alioutaja kuwa mbaya na haufai akisema mfumo huo utalemaza maendeleo ya ugatuzi katika baadhi ya kaunti nchini, hasa kutokana na suala la idadi ya watu na vigezo vya umasikini.
“…Ukipiga hesabu pesa tunayopasa kupata sasa kwa mfumo ule wa mgao wanaopendekeza wao takribani zaidi ya 250 itakuwa imepungua Mombasa, kasha kaunti nyingine ambazo zinapata mabilioni izidi kupata mabilioni zaidi.
Hii si kichocheo cha ugatuzi, ugatuzi si kusema kuzidi kushabikia umaskini, ugatuzi ni kujaribu kuhakikisha kila kaunti inapiga hatua, maana sasa kila mmoja atatamani kuwa na kaunti maskini ili watamani kupata mgao zaidi.” Alisema.
Nassir alisema kigezo cha idadi ya watu na raslimali au taasisi haipaswi kutumika kwa kuwa wanaoingia mjini Mombasa na kutumia raslimali kama vile hospitali ni wengi ikilinganishwa na takwimu za idadi ya watu iliyofanyika wakati wa usiku.
Gavana huyo hata hivyo ameeleza matumani yake kutupiliwa mbali mapendekezo ya mfumo huo mpya wa ugavi pale yatakapofikishwa katika Bunge la Seneti huku akifichua kua magavana watakutana kujadili zaidi hatima yake hiyo.
“Hakuna formula mbovu kama waliyopendekeza safari hii, na tutaitana kikao kama viongozi kuweza kupinga hii pendekezo walioileta na nina imani Seneti pia watakataa huu mpango walioweza kuuleta.” Akaongeza.
Haya yanajiri huku ikibainika kuwa huenda zaidi ya kaunti 20 zikaathirika kwa kupata mgao mdogo wa mapato ukilinganisha na mgao wa hapo awali iwapo mfumo mpya huo unaopendekezwa na Tume ya Ugavi wa Mapato, CRA utaidhinishwa na Bunge.
Katika mapendekezo hayo ya mfumo mpya wa ugavi wa mapato, Mkuu wa CRA, Mary Chebukati amesema kaunti zenye idadi kubwa ya watu zitapokea mgao zaidi huku idadi ya watu ikikadiriwa kuwa asilimia 42 kutoka asilimia 18 katika mfumo wa
sasa wa ugavi wa mapato. Katika msingi wa tatu, mfumo uliopitishwa mwaka 2020 wa ugavi wa mapato uliweka ugavi kwa kukadiria idadi ya watu kuwa asilimia 18 na sasa imependekezwa kuongezeka hadi asilimia 42, Sehemu sawa ya mgao kwa sasa ni asilimia 20 ambayo imependekezwa kupanda hadi asilimia 22.
Licha ya kwamba kigezo cha asilimia 42 ya idadi ya watu kinaegemea kaunti zenye idadi kubwa ya watu baadhi ya kaunti zilizo na idadi ndogo ya watu zitanufaika na mgao zaidi kutokana na vigezo vya viwango vya umaskini na kiwango cha ukubwa wa ardhi.
Mfumo huo mpya sasa utapunguza mapato kwa kaunti 31, huku Kitui ikitarajiwa kupoteza shilingi milioni 343, huku Narok ikipoteza shilingi milioni 310 katika mgao ujao.
Kaunti za Kitui, Kakamega na Narok ni miongoni mwa zile zitakazoathirika pakubwa na pungozo la mgao wao wa mapato katika mapendekezo hayo mapya. Kaunti ya Kakamega ndiyo itkayoathirika zaidi na punguzo la mapato katika ugavi huo huku kaunti za Machakos, Kilifi, na Meru zikipoteza zaidi ya shilingi 250 iwapo bunge la Seneti litaidhinisha mfumo huo.
Mapendekezo hayo tayari yametumwa katika Bunge la Seneti ilinkuzingatiwa huku baraza la magavana likitarajiwa kukutana kutathmini na kuchukua msimamo kuhusu mfumo huo mpya wa ugavi.Ikumbukwe kuwa kikatiba Mfumo wa kubadilisha mgao wa fedha na Tume ya Ugavi wa Mapato CRA, kwa serikali za kaunti hufanywa kila baada ya miaka 5.
By Mjomba Rashid