Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya amemsuta Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah kwa kumhusisha na vifo na utekaji nyara
wakati akiwa Mkuu wa Mkoa wa Bonde la Ufa katika utawala ra serikali iliyopita.
Katika taarifa yake Ijumaa jioni Gavana Natembeya amelaani vikali mashambulizi ya maneno yaliyoelekezwa kwake na Ichung’wah, na kuyataja kuwa ya upumbavu na ya aibu.
Amejitenga mbali na madai yaliyomhusisha na miili iliyopatikana imetupwa Mto Yala mnamo mwaka 2022, akisisitiza kwamba muda wake kama Mkuu wa Mkoa wa Bonde la Ufa haukuwa na kashfa na kwamba alistaafu bila lawama baada ya muhula wake.
Gavana huyo ametetea tajriba ya uongozi wake kama kama kiongozi aliyehitimu na mwenye bidii, na kuongeza kuwa rekodi yake ya utendajikazi ilimfanya kuchaguliwa kwake kuwa Gavana wa Trans Nzoia.
“Ifahamike kwamba George Natembeya alihudumu kama mtumishi mwenye bidii, mwaminifu, na mwaminifu kwa watu wa Kenya. Nafasi niliyoipata kupitia sifa na bidii. Nilijiuzulu ukuu wa Mkoa bila doa wala kashfa yoyote,” alisema. "Kujitolea kwangu kama Kamishna wa Mkoa kumenifanya nipendezwe na watu mashuhuri wa Trans Nzoia, ambao walinilea na kuwa gavana wao wa pili.”
Natembeya amewakashifu viongozi washirika wa Kenya Kwanza kwa kile alichokitaja kuwa wanaelekeza hasira zao kwake badala ya kuangazia kiini na tatizo lililopo la kumaliza wimbi la hivi punde la visa vya utekaji nyara na mauaji yalioibua ghadhabu kwa Wakenya.
Ameeleza kukwerwa na jinsi alivyokashifiwa na kusutwa Na Ichungwa’h kwa kumshinikiza Rais William Ruto kuwajibikia suala la utekaji nyara na kutoweka kwa vijana, jambo analosema ni jukumu la kila kiongozi na haipaswi kudhaniwa kuhujumu walio mamlakani.
By Mjomba Rashid