HabariNews

Rais Ruto Aomboleza Kifo cha Mwenyekiti wa Tume ya (KNCHR) Roseline Odede

Rais Ruto Aomboleza Kifo cha Mwenyekiti wa Tume ya (KNCHR), Roseline Odede Aliyefariki baada Ugonjwa wa Muda mfupi Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KNCHR) imetangaza kufariki kwa Mwenyekiti wake, Roseline Odhiambo Odede, baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na Naibu Mwenyekiti wa KNCHR Dkt. Raymond Nyeris, Bi. Odede aliaga dunia jana Ijumaa baada ya kuugua kwa muda mfupi.

"Ni kwa mshtuko na huzuni kubwa ninawajulisha kuhusu kifo cha Roseline Odhiambo Odede, HSC, Mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya

Kenya, kilichotokea jana, Ijumaa, Januari 3, 2025, baada ya kuugua kwa muda mfupi," ilisema sehemu ya taarifa hiyo.

Tume hiyo imeomboleza kifo chake ilichokitaja kuwa pigo kubwa kwa shirika hilo la kutetea haki za binadamu nchini na pia pigo kwa taifa zima kwa jumla.

Taarifa hiyo ya KNHCR imebaini kushtushwa na habari za kifo chake hicho huku ikitoa risala zake za rambirambi kwa familia na marafiki wa Bi. Odede, ikitambua pengo kubwa lililotokana na kifo chake.

Rais William Ruto mnamo Jumamosi aliongoza Wakenya kumwomboleza Mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu, Roseline Odede.

Katika mtandao wake wa X Rais alituma risala zake za rambirambi akieleza kuhuzunishwa na kifo cha Odede, akimtaja Bingwa imara wa haki za kibinadamu na mwanaharati mashuhuri aliyepigania usawa na haki katika jamii.

“Nimehuzunishwa sana na kifo cha Mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya Roseline Odhiambo Odede.

Alikuwa bingwa imara wa haki za binadamu na mwanaharakati mashuhuri aliyepigania usawa na haki katika jamii. Mawazo na upendo wetu uko pamoja na familia katika wakati huu wa huzuni.” Ulisema ujumbe wa X ya Rais Mipango ya mazishi kwa sasa bado haijatangazwa.

By Mjomba Rashid