HabariNews

Wabunge ukanda wa Pwani walaumiwa kwa visa vya wanafunzi kukosa ufadhili wa kuendeleza masomo yao Pwani

Viongozi wanaendelea kunyosheana kidole cha lawama kufuatia kubainika kuwa baadhi ya wanafunzi wanaoshindwa kuendeleza masomo yao hukosa ufadhili wa masomo, lawama kubwa ikielekezwa kwa wabunge ukanda wa Pwani.

Viongozi ukanda wa pwani hasa wabunge kwenye kundi la “Coast Parliamentary Group” wamenyoshewa kidole cha lawama kufuatia visa vingi vya vijana kushindwa kuendeleza masomo yao kutokana na ukosefu wa ufadhili wa masomo yao.

Kwa mujibu wa George Kithi aliyekuwa mgombea wa ugavana kaunti ya Kilifi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2022, vijana wamekuwa wakipitia hali ngumu za kuendeleza masomo yao kutokana na viongozi wengi ukanda wa pwani kuwa wabinafsi na kutolipa kipaumbele swala la elimu.

Vile vile ameeleza kusikitishwa kwake na viongozi wa “Coast Parliamentary Group” kufeli kutafuta suluhu ya matatizo ambayo yamekuwa yakiwakumba wanafunzi pwani kwa zaidi ya miongo miwili huku akisema kuwa viongozi wameelekeza fikra zao kwenye kujipatia umaarufu pekee.

Hapana. Haiwezi kwasababu hawa viongozi hawafikirii zaid. Tangulizi ya fikra nadhani ni kwa kiasi gani naweza kuwa maarufu kutunga sheria badala ya kutafuta suluhu ya hii changamoto, kwanini hatuvioni hivyo? Ukweli ni kwamba kuna uchoyo na ubinafsi mwingi na kutoaminiana. Mgawanyiko kuliko kile kinachoweza kutuunganisha na kisha tunajiita wapwani ambao huu ni ujinga mtupu.

“Hatujaona chochote kwa “Coast Parliamentary Group” ambacho kimemsaidia kijana wa pwani kuendeleza masomo yak. Matatizo tuliyokuwa nayo miaka ishirini iliyopita ni yale yale yanayowakumba vijana wetu. Hatuwezi kamwe kuuamini uongozi wetu, kuna jambo linafaa kubadilika.” alisema Kithi.

Kwa upande wake mbunge wa Kilifi kaskazini Owen Baya amekashifu madai hayo akieleza kuwa kuna mchango mkubwa aliofanya kwenye sekta ya elimu kaunti ya Kilifi.

Aidha amesistiza kuwa wale wanaolalamika kuhusu viongozi kufeli kuwajibikia maswala ya elimu wanafaa kuonesha hatua walizopiga katika kurekebisha changamoto hiyo badala ya kuongea maneno ya kukashifu ili kujipatia umaarufu.

Nikimskia George Kithi anaongea kuhusu maswala ya elimu huwa nahisi si mtu sahihi wa kuongelea swala hili. Kithi amekuwapo miaka yote hiyo kabla hata mimi sijakuwa mbunge niliwacha alama kwenye sekta ya elimu hapa Kilifi,na wapo watu wengi ukiwauliza watakwambia nilichofanya wakati nikiwa raia wakawaida. Uwekezaji ambao nimefanya ndani ya kaunti ya Kilifi kuhusu elimu ni mkubwa sana. Je, yeye amefanya kitu gani cha kuonesha kuwa anajali maswala ya elimu ndio atukashifu kuhusu elimu?

“Unajua usije na kuanza kuropoka maneno eti kwasababu unatafuta umaarufu. George Kithi hana mwelekeo wa kisiasa wala kimaendeleo. Kitu pekee anachotaka ni mamlaka.” alisema Baya.

Erickson Kadzeha.