Mamlaka ya Kudhibiti Kawi na Petroli (EPRA) imetangaza ongezeko la bei za mafuta ya Petroli, Dizeli na Mafuta ya Taa kuanzia Januari 15 hadi Februari 14, 2025.
Katika taarifa iliyotolewa Jumanne, Mkurugenzi Mkuu wa EPRA Daniel Kiptoo, amesema Super Petrol itaongezeka kwa shilingi 0.29, Dizeli kwa shilingi 2, na Mafuta ya Taa kwa shilingi 3 kwa lita.
Kufuatia ukaguzi huo, lita moja ya Super Petrol jijini Nairobi sasa itauzwa kwa shilingi 176.58, Dizeli shilingi 167.06 na Mafuta ya Taa kwa shilingi 151.39.
Mjini Mombasa, Super Petrol itauzwa kwa shilingi 173.34, Dizeli shilingi 163.82, na Mafuta ya Taa shilingi 148.15.
Mjini Kisumu, gharama za mafuta ya Super Petrol, Dizeli na Mafuta ya Taa zitakuwa shilingi 176.62, shilingi 167.44, na shilingi 151.82 mtawalia.
Kulingana na EPRA bei hizo mpya ni pamoja na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya asilimia 16% kwa mujibu wa masharti ya Sheria ya Fedha ya 2023, Marekebisho ya Sheria ya Kodi ya 2024 na viwango vilivyorekebishwa vya Ushuru wa Bidhaa vilivyorekebishwa kwa mfumuko wa bei kwa mujibu wa Notisi ya Kisheria ya nambari 194 ya 2020.
By Mjomba Rashid