Onyo kali imetolewa kwa wafanyakazi wa idara ya afya kaunti ya Kilifi kuwa hatua kali za sheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote anayejihusisha na wizi wa dawa pamoja na vifaa vingine vya matibabu, hatua hii ikilenga kuimarisha huduma kwa wakazi.
Onyo hiyo imetolewa kufuatia lalama zinazotolewa mara kwa mara na wakazi kwamba wamekuwa wakikosa dawa wanapotafuta huduma za matibabu katika hospitali za umma kaunti ya Kilifi.
Kwa mujibu wa waziri wa afya kaunti ya Kilifi Peter Mwarogo, changamoto ya kukosekana kwa dawa katika hospitali za umma imekithiri licha ya juhudi za serikali kuhakikisha kuwa inagawa dawa za kutosha katika taasisi za matibabu ya umma.
Akitoa onyo hiyo Mwarogo ameeleza kuwa sheria haitamsaza mfanyakazi yeyote anayejihusisha na visa vya wizi wa dawa huku akitoa wito kwa wakazi kutoa taarifa wanaposhudia vitendo kama hivi ili kukomesha kuendelea kwa visa hivyo vya wizi.
“Tunataka kuwaambia ni onyo hasa kwa wafanyakazi wanaohusika na mambo kama haya, na pia tungetoa wito kwa wananchi wawe macho wanaopoona kitu kama hicho wanatufahamisha haraka iwezekanavyo ili tuweze kuwakamata watu hao na kuwachukulia hatua za sheria.
“Tumekuwa tukishangaa sana manake kila wakati tunagawanya dawa katika hospitali zetu lakini mara kwa mara tumekuwa tukipata malalamishi kutoka kwa wananchi kwamba dawa hazitoshi na sasa tumejuwa hasa ni nini ambacho hufanyika. Ni kwamba kuna baadhi ya wafanyakazi ambao wanaiba dawa kwa hivyo tunachukuwa hatua kuhakikisha kwamba hili litakuwa funzo na onyo kwa wengine.” alisema Mwarogo.
Mkuu wa polisi eneo bunge la Kilifi kaskazini Kennedy Maina amewashukuru wakazi kwa kutoa taarifa na kuwahimiza kujihisi huru na kutoa taarifa muhimu zitakazosaidia kukomesha visa vya wizi huo wa dawa.
“Nataka kuwashukuru wananchi, na aliyetuletea ujumbe na kutuambia ni kweli kuna mahali kumeonekana kuna dawa zinapelekwa. Na vile vile niwahimize wananchi tuko tayari mutuletee ujumbe, musituogope tunawakikishia faragha na hizo habari tutazifanyia kazi ili tuweze kuwasaidia wananchi.” alisema Maina.
Hayo yanajiri siku chache baada ya baadhi ya wafanyakazi wa idara ya afya kaunti ya Kilifi kukamatwa wakijihusisha na uuzaji dawa za wizi kutoka serikali katika duka moja la kibinafsi la kuuza dawa eneo la Bamba.
Erickson Kadzeha