Waziri wa Utumishi wa Umma Justin Muturi amepasua mbarika katika ufichuzi mkali wa jinsi mwanawe, Leslie Muturi, alivyodaiwa kutekwa nyara na kuachiliwa na maafisa wa Ujasusi (NIS) kufuatia agizo la Rais William Ruto.
Katika taarifa kwa polisi aliyoirekodi leo Jumanne huko Kilimani, Waziri huyo ametoa maelezo ya kina kuhusu jinsi mwanawe alivyotekwa nyara mnamo Juni 22, 2024, na majambazi waliokuwa wamejihami kwa silaha kwenye Barabara ya Dennis Pritt.
Kulingana na maelezo ya Waziri Muturi mwanawe Leslie alikuwa pamoja na Mbunge wa Embakasi Magharibi Mark Mwenje na Marangu Imanyara katika Mgahawa wa Alfajiri Lounge kabla ya kuamua kwenda kwenye sherehe ya kuzaliwa huko Lavington.
Muturi kwenye taarifa yake kwa polisi ameeleza mahangaiko aliyopitia kumsaka mwanawe kuanzia kuwapigia simu Inspekta Jenerali wa Polisi wakati huo Japhet Koome na Katibu Mkuu wa Usalama wa Ndani Raymond Omollo, ambao waliahidi kuangazia suala hilo.
Hata hivyo amedai juhudi zake za kuwasiliana na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Jinai (DCI) Mohammed Amin na Mkurugenzi Mkuu wa NIS Noordin Haji ziliambulia patupu kwani simu zake ziliita bila kupokelewa, huku aidha ujumbe wa Whatsapp aliomwandikia Rais akidai kutosomwa kamwe.
Waziri huyo amesema alimpigia tena Koome ambaye alimhakikishia kwamba alikuwa amewaarifu wafanyakazi wote katika njia zote, akishuku kuwa huenda ulikuwa wizi licha ya kutiwa hatiani kwa Muturi kwamba ilikuwa operesheni ya polisi.
Aidha Muturi ameeleza kuwa baada ya mahangaiko hayo alimwandika ujumbe wa Whatsapp Rais William Ruto kuhusu kutekwa nyara kwa mwanawe na alipoona haujasomwa alifunga safari hadi Ikulu ya Nairobi alikokutana ana kwa ana na rais na kumweleza kuhusu suala hilo.
Alimtaka Rais ampigie simu Mkurugenzi wa NIS na rais alifanya hivyo ambapo Muturi amedai alimsikia Rais akimuuliza Noordin Haji iwapo alimkamata mwanawe Leslie, na Noordin alithibitisha kukamatwa kwake kabla ya kuagizwa amwachilie mara moja naye Noordin akiahidi kumwachilia katika muda waa saa moja.
“Nikiwa nimesimama nje, nilimsikia Rais akimuuliza Haji kama anamshikilia mwanangu, Noordin alithibitisha kwamba ni kweli alikuwa amemkamata mwanangu na Rais alimuagiza amwachie Leslie mara moja.” Muturi alisema kwenye taarifa yake.
Muturi alikiri kuwa mwanawe baadaye aliachiliwa na kwenda nyumbani.
By Mjomba Rashid