Kizaazaa kimeshuhudiwa katika afisi za Wizara ya Afya jijini Nairobi baadhi ya wakenya walipovamia afisi hizo kulalamikia mahangaiko na pandashuka tele za matibabu kupitia bima ya Afya ya jamii, SHA.
Wagonjwa wenye ghadhabu wamevuruga kikao cha maafisa wa Wizara ya afya na wahanahabari wakilalalamikia kukwama katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta ambako walikuwa wameenda kupata huduma za matibabu.
Wagonjwa hao wamevamia jengo la Afya House jiini Nairobi kulalamikia kushindwa kwa mfumo wa afya ya kijamii ya sha huku wakitaka majibu kutoka kwa waziri wa afya Deborah Barasa baada ya jitihada zao za kutaka kupata huduma kugonga mwamba na kuachwa bila msaada wowote.
Miongoni mwa wagonjwa hao ni mama wa mtoto wa siku 3, ambaye alikuwa ametoka kufanyiwa upasuaji.
“Baadhi ya watu wametoka Kibwezi na wengine wametoka Mombasa; SHA haifanyi kazi na hawaidhinishi. Kuanzia Jumatano wiki jana wanasema mifumo iko chini, systems ziko chini mbona kwenye malipo tunalipa na systems hazifeli haziwi chini?” mgonjwa alilalamika.
Haya yanajiri huku Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) ikijitokeza kuangazia lalama hizo za kucheleweshwa kwa huduma kutokana na kukatika kwa mifumo ya Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA).
Katika taarifa yake mnamo Jumatano, Mkurugenzi Mtendaji wa hospitali hiyo Dkt. Evanson Kamuri aliomba radhi kwa hitilafu ya kiufundi iliyoathiri mifumo ya SHA ambayo ilisababisha wagonjwa kuvamia ofisi za Wizara ya Afya kudai majibu.
Dkt. Kamuri alisema kuwa changamoto hizo za siku mbili tayari zimepatiwa uvumbuzi na kwamba shughuli zimerejea katika hali ya kawaida.
“Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta (KNH) inapenda kukiri kudorora kidogo kwa huduma ya wagonjwa leo na kuwahakikishia umma kwamba mfumo wa Mamlaka ya Afya ya Kijamii (SHA) sasa unafanya kazi kikamilifu na unaambatana na mfumo wa KNH. Operesheni za kawaida zimeanza tena, na wagonjwa wanahudumiwa,” alisema.
Katika lengo la kushughulikia kesi hizo, KNH ilisema kuwa wafanyakazi zaidi wamewekwa na watafanya kazi kwa muda wa ziada kuhakikisha kesi zote zimeshughulikiwa.
By Mjomba Rashid